
KIONGOZI wa chama cha upinzani cha NUP nchini Uganda, Bobi Wine amekubali mwaliko wa mkuu wa majeshi Muhoozi Kainerugaba ambaye ni mwanawe rais Museveni la kutaka wapigane.
Kainerugaba, ambaye amekuwa akionyesha waziwazi chuki yake
dhidi yam wanasiasa huyo alitoa wito kwake akimtaka kumjaribu katika mduara wa
vita ikiwa kweli anaona atammudu.
Muhoozi, ambaye kwa sasa ameifunga akaunti yake ya X, alisema
kwamba kwa vile Bobi Wine amekuwa akidai kuwa shabiki na mpenzi mkubwa wa
mchezo wa ngumi, basi amjaribu yeye katika pambano moja.
“Anasema anapenda mchezo
wa masumbwi, basi namwalika kwa pambano la ngumi,” Muhoozi Kainerugaba
alichapisha.
Bobi Wine kwa ujasiri alimjibu akitanguliza na Kauli ya
kijasiri kwamba amekubali mwaliko huo huku akimtaka Kainerugaba kutangaza
tarehe na na yeye atatangaza sehemu ya kufanyika kwa mchuano wao.
Hata hivyo, Bobi Wine alikubali pambano hilo kwa masharti kwa
mkuu huyo wa majeshi akisema kwamba ikiwa Muhoozi atamshinda basi yuko radhi
kuachana na siasa kabisa.
Pia, Wine alisema kwamba sharti lingine kwa Muhoozi ni
kukubali kuacha pombe ikiwe atamshinda katika pambano hilo.
“Nimekubali mwaliko kwa pambano. Kama utanishinda nitaachana kabisa na siasa, lakini kama nitakushinda itabidi umeachana na pombe. Sema ni lini na mimi nitasema ni wapi,” Bobi Wine alisema.
Muhoozi amekuwa akichapisha jumbe la kutishia maisha ya Bobi
Wine, mara nyingi akimrejelea kwa jina la utani la ‘Kabobi’.
Mwezi Januari mwaka huu, Kainerugaba alichapisha ujumbe wa
kutaka kumuadhibu Bobi Wine, akisema kwamba mtu pekee anayezuia adhabu hiyo
kufanyika ni baba yake, rais Yoweri Museveni.
Ni ujumbe ambao uliibua wasiwasi ya Bobi Wine ambaye alisema
kwamba jaspo ulionekana kuwa wa utani lakini ulikuwa unahusishwa na kutamatisha
maisha yake huku akimkashifu Muhoozi kwa kutumia mamlaka yake visivyo.
“Kabobi anajua kwamba mtu pekee anayemlinda kutoka kwangu
ni babangu. Kama mzee wangu hangekuwa, ningekata kichwa chake leo,” Muhoozi aliandika.
“Tishio la mtoto wa Museveni (ambaye pia anaongoza jeshi
la Uganda) la kunikata kichwa si jambo ninalolichukulia kirahisi, ikizingatiwa
kwamba wengi wameuawa na yeye na baba yake, na kwa kuzingatia majaribio yao
kadhaa ya kuniua. NIKATAA kutishwa na utawala waoga. Ulimwengu unatazama,” Wine alijibu akinukuu chapisho hilo la
Kainerugaba.