
Msanii na mwanasiasa wa upinzani nchini Uganda, Bobi Wine, ameachia wimbo mpya unaoitwa Third Time Lucky, akitoa wito wa kuachiliwa kwa kiongozi wa upinzani, Dkt. Kizza Besigye, na wafungwa wengine wa kisiasa nchini humo.
Kupitia ujumbe wake wa kutangaza wimbo huo, Bobi Wine alisema:
"Huu hapa ni wimbo tuliorekodi wiki iliyopita kwa ushirikiano na @BrenthurstF ili kuongeza uelewa kuhusu kuzuiliwa kwa Dkt. Kizza @kizzabesigye1 na wafungwa wengine wa kisiasa! Unaweza kuutazama kwenye YouTube na majukwaa mengine."
Wine aliendelea kufafanua kuwa wimbo huo ulirekodiwa jijini Kampala, Uganda, mnamo Februari 2025, ukiwa ni wito wa "ukombozi wa tatu wa Afrika". Uliandikwa na Robin Auld na Greg Mills, pamoja na Paddyman.
Kwa mujibu wa Bobi Wine, Third Time Lucky umetolewa ili kuangazia suala la kutekwa kwa Besigye nchini Kenya na kushtakiwa kwake katika mahakama ya kijeshi.
Mke wa Besigye, Winnie Byanyima, ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa UNAIDS, alisifu juhudi za Bobi Wine kwa kuimba wimbo huo.
"Wimbo huu unatoa mwito wa ukombozi wa tatu wa Afrika na unajumuisha sauti za demokrasia kutoka duniani kote zinazodai 'Free Kizza'. Miongoni mwao ni mshindi wa Tuzo ya Nobel Oleksandra Matviichuk, marais wa zamani Ellen Johnson Sirleaf, Andrés Pastrana, Martin Torrijos na Ian Khama, mawaziri wakuu wa zamani Yulia Tymoshenko na Moeketsi Majoro, Askofu Mkuu wa Cape Town Thabo Makgoba, pamoja na mawaziri na viongozi wa upinzani kutoka Afrika, Amerika ya Kusini na Ulaya," Byanyima alisema kupitia Twitter.
Katika ujumbe mwingine, mkewe Besigye alimshukuru Bobi Wine kwa mchango wake katika kupigania haki za kisiasa.
"Asante @HEBobiwine kwa kuunda wimbo unaoitaka dunia kudai kuachiliwa kwa @kizzabesigye1 na wafungwa wengine wote wa kisiasa. Sisi sote ni mateka wa dikteta na mwanawe. Tutajikomboa," alisema.
Kizza Besigye, mpinzani wa muda mrefu wa Rais Yoweri Museveni, amekumbwa na mateso na kukamatwa mara kadhaa kutokana na msimamo wake mkali dhidi ya serikali.
Kukamatwa kwake mwaka jana na kesi inayomkabili katika mahakama ya kijeshi imeibua wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya demokrasia nchini Uganda.
Wimbo wa Third Time Lucky unatarajiwa kuwa moja ya nyenzo muhimu za harakati za kimataifa zinazodai uhuru wa Besigye na mageuzi ya kisiasa nchini humo.