
Kampuni ya usafiri wa abiria, Super Metro Limited, imesitisha huduma zake kwa siku tatu kuanzia Jumatatu, Aprili 14.
Kusitishwa huko kumetokana na agizo la Bodi ya Rufaa ya Leseni za Usafiri (TLAB) baada ya kikao maalum kilichofanyika Jumatatu.
Katika taarifa iliyotolewa Jumatatu jioni, Super Metro ilieleza kuwa imekamilisha asilimia 90 ya masharti ya usalama na uendeshaji yaliyoagizwa na Mamlaka ya Kitaifa ya Usalama wa Usafiri (NTSA) pamoja na TLAB.
Kusitishwa kwa huduma kwa sasa kunalenga kutoa nafasi ya kukamilisha asilimia iliyosalia ili huduma zote ziendane kikamilifu na sheria.
"Baada ya kikao na Bodi ya Rufaa ya Leseni za Usafiri leo, Bodi imeagiza Super Metro kusitisha huduma kwa siku tatu zijazo ili kukamilisha masharti yaliyosalia," ilisema kampuni hiyo kupitia taarifa rasmi.
Super Metro imesisitiza kuwa inaheshimu uamuzi huo wa TLAB na mahakama, na tayari inaendelea kushughulikia masuala yaliyosalia.
"Tunafanya kazi kwa bidii kuhakikisha tunatimiza masharti hayo kwa muda tuliopangiwa. Tutarejelea huduma mara tu tutakapopata idhini kutoka kwa mamlaka husika," taarifa hiyo ikaongeza.
Kulingana na NTSA, kusimamishwa kwa kampuni hiyo kwa mara ya kwanza kulifanyika Machi 20, kutokana na ukiukaji wa masharti ya usalama.
Hata hivyo, mahakama baadaye iliondoa zuio hilo kwa muda, huku kampuni ikiendelea kushughulikia masharti yaliyotolewa.
Miongoni mwa changamoto zilizobainishwa na NTSA ni magari kuwa na vyeti vya ukaguzi vilivyomaliza muda wake, leseni zilizopitwa na wakati, vyeti vya vizuia mwendo (speed limiters) ambavyo havikuwa halali, pamoja na kukosekana kwa taarifa kamili za vifaa hivyo.
Pia, baadhi ya madereva walidaiwa kukosa sifa zinazotakiwa kisheria. NTSA ilitaka kampuni hiyo kuwasilisha magari 294 kwa ukaguzi mpya, pamoja na kupeleka madereva 42 waliobainika kuvunja sheria za mwendo kwa majaribio ya upya katika kituo cha Likoni.
“Madereva 64 walifeli majaribio hayo ya Machi 10, hali iliyopelekea leseni zao kusitishwa,” NTSA ilieleza.
Super Metro imewaomba radhi abiria wake kwa usumbufu unaoweza kusababishwa na kusitishwa kwa huduma. Imesisitiza kuwa inaendelea kujitolea kutoa usafiri salama, wa kuaminika na unaozingatia sheria.
Kwa taarifa zaidi, wateja
wanahimizwa kuwasiliana kupitia barua pepe [email protected] au kupiga simu 020
2522873.