
Jopo la Rufaa la Leseni za Usafiri (Transport Licensing Appeals Board - TLAB) limeamuru Sacco ya Super Metro kuwatimua mara moja na madereva wake 269, kutokana na ukiukaji wa kanuni za usalama barabarani. Uamuzi huo umetolewa baada ya kikao kati ya Super Metro na Mamlaka ya Kitaifa ya Usafiri na Usalama Barabarani (NTSA).
Kwa mujibu wa agizo hilo, majina ya madereva wanaopaswa kuachishwa kazi yameorodheshwa kwenye hati iliyowasilishwa na NTSA tarehe 10 Aprili, 2025. Jopo hilo limeelekeza kuwa madereva hao waachishwe kazi bila kuchelewa.
Mbali na hatua hiyo, Super Metro pia imeamuriwa kupeleka magari 31 yaliyoonekana kuwa na changamoto za utii wa viwango kwa ukaguzi katika Kituo cha Ukaguzi wa Magari cha Likoni.
Baada ya ukaguzi huo, Sacco hiyo inatakiwa kuwasilisha ripoti za ufuatiliaji wa utekelezaji kwa Kurugenzi ya Usalama ya NTSA.
Vilevile, magari 42 yaliyobainika kuvunja sheria za mwendokasi yameamriwa kurudishwa kwenye Kituo cha Mitihani cha Madereva cha Likoni kwa ukaguzi upya.
Jopo hilo pia limeamuru magari manane ambayo yana matatizo yanayohusiana na vifaa vya kudhibiti mwendokasi (speed limiters) yakaguliwe mara moja katika Kituo cha Ukaguzi wa Magari cha Likoni.
Zaidi ya hayo, Super Metro imetakiwa kuwasilisha kwa NTSA nakala ya kumbukumbu za vikao vya uhamasishaji wa usalama barabarani kwa madereva wake, pamoja na orodha ya waliokuwepo kwenye vikao hivyo.
Aidha, jopo hilo limeagiza kurejeshwa kwa agizo la awali la NTSA la kusimamisha huduma zote za Sacco hiyo hadi itakapothibitishwa kuwa imezingatia masharti yote yaliyoainishwa. Kesi hiyo itatajwa tena tarehe 17 Aprili, 2025, kwa ajili ya kuthibitisha utekelezaji na kutoa maelekezo mengine.
Agizo hili linakuja siku moja tu baada ya Super Metro kutangaza kwamba ingesitisha huduma zake kwa muda wa siku tatu. Sacco hiyo ilidai kuwa tayari imetekeleza asilimia 90 ya maagizo yaliyotolewa na NTSA na TLAB
Mnamo tarehe 20 Machi, 2025, Super Metro ilisimamishwa shughuli zake ili kuruhusu utekelezaji wa hatua za kiusalama. Hata hivyo, siku chache baadaye, jopo hilo lilisitisha kwa muda agizo hilo na kuruhusu magari yao kurejea barabarani huku utekelezaji wa masharti ukiendelea kufuatiliwa.