

Mwili wa Papa Francis kwa sasa umewekwa katika Kanisa la Santa Marta ndani ya jiji takatifu la Vatican, ambako waumini na waombolezaji wanapewa fursa ya kumtolea heshima zao za mwisho.
Kwa mujibu wa mapenzi yake ya mwisho, mwili wake umevalishwa mavazi kamili ya Kipapa na kuwekewa rozari mikononi mwake.
Badala ya kuwekwa juu ya jukwaa la heshima (bier) kama ilivyo desturi, mwili wake umehifadhiwa katika jeneza rahisi la mbao lenye tabaka la zinki badala ya mvinje, risasi, na mwaloni.

Hili linaonyesha hamu yake ya kuishi maisha ya unyenyekevu hadi mwisho wa maisha yake. Vatican imetoa picha na video za kwanza zikionyesha hafla ya faragha iliyofanyika Jumatatu katika makazi ya Casa Santa Marta.
Wakati huo huo, makardinali kutoka kote duniani wamekusanyika mjini Vatican kupanga tarehe na utaratibu wa mazishi ya Papa Francis. Kwa mujibu wa Katiba ya Kitume inayojulikana kama Universi Dominici Gregis, makardinali wote wa Baraza la Kimataifa wanaruhusiwa kuhudhuria mikutano ya kila siku ya maandalizi (General Congregation).

Katika mchakato wa kuchagua Papa mpya, makardinali walioteuliwa na Papa ambaye amefariki — na ambao hawajafikisha umri wa miaka 80 — wanahitajika kukusanyika kwa ajili ya kikao maalum kinachojulikana kama conclave. Hadi sasa, kuna jumla ya makardinali 136 waliostahiki kushiriki, lakini ni 120 pekee wanaoruhusiwa rasmi kupiga kura katika uchaguzi huo.
Hata hivyo, kabla ya kikao hicho cha uchaguzi kuanza, ni lazima makardinali hao wakubaliane kwanza kuhusu tarehe ya mazishi ya Papa Francis, na kisha waamue tarehe rasmi ya kuanza kwa conclave.
Kipindi rasmi cha maombolezo hujulikana kama Novendiales, na huchukua siku tisa. Kwa mujibu wa mila za Kanisa Katoliki, mwili wa Papa huzikwa kati ya siku ya nne na ya sita tangu kifo chake. Kipindi hiki cha mpito kati ya kifo cha Papa na kuchaguliwa kwa mrithi wake hujulikana kama Papal Interregnum.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Vatican, mwili wa Papa Francis unatarajiwa kuhamishiwa hadi katika Basilika ya Mtakatifu Petro siku ya Jumatano, ili kutoa nafasi kwa umma kumuaga. Baada ya kumalizika kwa kipindi cha maombolezo, Misa kuu ya mazishi itaandaliwa kwenye basilika hiyo hiyo kama sehemu ya heshima ya mwisho kwa kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki.