
Mazishi ya Papa Francis yatafanyika Jumamosi katika uwanja wa St Peter's Square, Vatican imethibitisha, huku mamia kwa maelfu wakitarajiwa kuhudhuria.
Mkuu huyo wa Kanisa Katoliki alifariki kutokana na maradhi ya kiharusi siku ya Jumatatu, akiwa na umri wa miaka 88, chini ya saa 24 baada ya kuongoza hotuba ya Pasaka. Afya yake ilizorota baada yakukabiliwa na homa kali ya mapafu hivi karibuni.
Viongozi kadhaa duniani wamethibitisha kuhudhuria mazishi yake ikiwa ni pamoja na Waziri Mkuu wa Uingereza Sir Keir Starmer, Rais wa Marekani Donald Trump, Mwana wa Mfalme wa Wales, na Rais Luiz Inácio Lula da Silva wa Brazil.
Maelfu ya waombolezaji tayari wamemiminika katika jiji la Vatican, wakiwa wamebeba maua, misalaba na mishumaa na kukariri sala.
Siku ya Jumanne, Vatican ilitoa maelezo zaidi ya saa 24 za mwisho za Papa.
Francis, ambaye alikuwa amelazwa hospitalini kwa wiki tano hivi karibuni, hakuwa na hofu ya kujitokeza kwenye roshani siku ya Jumapili.
"Unafikiri ninaweza kufanya hivi?" Papa alimuuliza muuguzi wake binafsi, Massimiliano Strappetti.
Strappetti alimtuliza na muda mfupi baadaye papa akatokea kwenye roshani, akiubariki umati uliokusanyika katika Uwanja wa St Peter's.
Asubuhi iliyofuata karibu 05:30 saa za ndani (03:30 GMT), Papa Francis alianza kujisikia vibaya. Saa moja baadaye, alimpungia Strappetti kabla ya kupoteza fahamu.
"Wale waliokuwa karibu naye katika nyakati hizo wanasema hakuteseka," Vatican ilisema katika taarifa yake. "Ilikuwa kifo cha utulivu."
Nini kitatokea kabla ya mazishi?
Siku ya Jumatano asubuhi, mwili wa Papa Francis utachukuliwa kwa maandamano yatakayoongozwa na makadinali kutoka Kanisa kuu la Santa Marta hadi Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, ambapo utakaa kwenye jeneza lililo wazi hadi Ijumaa ili kuruhusu waombolezaji kutoa heshima zao.
Muda mfupi kabla ya maandamano hayo, muda wa sala utaongozwa na camerlengo, Kadinali Kevin Farrell, ambaye anaiongoza Vatican baada ya kifo cha Papa.
Vatican imetoa picha za mwili wa Papa ukiwa umelazwa katika kanisa la Casa Santa Marta, makazi yake wakati wa utawala wake wa miaka 12, akiwa amevalia vazi jekundu na kilemba cha papa kichwani na rozari mkononi mwake.
Umma kwa ujumla utaweza kutembelea Basilica ya St Peter kutoka 11:00 hadi usiku wa manane siku ya Jumatano, 07:00 hadi usiku wa manane siku ya Alhamisi na 07:00 hadi 19:00 Ijumaa.
Ibada itafanyika saa ngapi?
Mazishi yataanza saa 10:00 katika uwanja ulio mbele ya Basilica ya St Peter.
Mababu, makadinali, maaskofu wakuu, maaskofu, na makasisi kutoka kote ulimwenguni watashiriki. Mkuu wa Chuo cha Makardinali, Kadinali Giovanni Battista Re, ndiye atakayeongoza ibada hiyo.
Kardinali Battista Re atatoa sala ya kuhitimisha ambapo Papa atakabidhiwa rasmi kwa Mungu na mwili wa Papa utahamishiwa St Mary Meja kwa maziko.
Kipindi cha maombolezo cha siku tisa, kinachojulikana kama Novemdiales, kisha kitaanza.
Nani anahudhuria mazishi?
Umati mkubwa unatarajiwa Jumamosi, na watu wengi kama 250,000 wanatarajiwa kuhudhuria mazishi.
Wakuu wengi wa nchi na familia ya kifalme wamethibitisha kuhudhuria kwao, akiwemo Mwanamfalme William, Rais wa Marekani Donald Trump, Mfalme wa Uhispania Felipe VI na Malkia Letizia na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron.
Viongozi wengine wa kisiasa ambao wametangaza kuwa watahudhuria ni pamoja na:
- Rais wa Brazil Luiz Inacio Lula da Silva
- Rais wa Poland Andrzej Duda
- Rais wa Tume ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen
- Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky
- Javier Milei, rais wa Argentina, nchi ya kuzaliwa kwa Francis
- Waziri Mkuu wa Uingereza Sir Keir Starmer
- Waziri Mkuu wa Italia Giorga Meloni
Papa Francis atazikwa wapi?
Papa Francis, ambaye aliepuka baadhi ya fahari za upapa wakati wa uhai wake, ataendelea kuvunja mila katika kifo.
Kihistoria, mapapa huzikwa katika majeneza matatu katika makaburi ya marumaru ndani ya Basilica ya Mtakatifu Petro katikati mwa Vatican. Papa Francis aliomba azikwe katika Kanisa kuu la Roma la St Mary Meja.
Atakuwa papa wa kwanza katika kipindi cha zaidi ya miaka 100 kuzikwa nje ya Vatican.
Katika wasia wake wa mwisho, Papa Francis pia aliomba azikwe ''bila mapambo maalum" na kwa maandishi tu ya jina lake la papa katika Kilatini: Franciscus.
Mwili wake ulihamishiwa katika kanisa la Santa Marta Jumatatu jioni, na nyumba yake kufungwa rasmi, Vatican ilisema.
Papa mpya atachaguliwa lini?
Kufuatia mazishi hayo, mkutano wa makadinali utafanyika ili kumchagua mrithi.
Mkuu wa Chuo cha Makardinali ana siku 15 hadi 20 kuwaita makadinali Roma mara tu Papa atakapozikwa.
Majina kadhaa tayari yameorodheshwa kama warithi wanaotarajiwa, na kuna uwezekano mkubwa wa kuibuka katika siku zijazo.