RAFIKI na mwandani wa msanii Diamond Platnumz, Baba Levo amefichua kwamba msanii huyo ana mpango kabambe wa kulisimamisha jiji kwa harusi yake na Zuchu.
Akizungumza na waandishi wa habari siku moja baada ya harusi
ya kipekee na mwanamitindo Hamisa Mobetto na mkwanasoka wa Yanga SC kutoka
Burkina Faso, Stephane Aziz Ki, Levo alisema kuwa Diamond ameanzisha mipango
kufanikisha jambo lake.
Chawa huyo alisema kuwa harusi ya Diamond na Zuchu itafanya
ile ya Hamisa Mobetto na Aziz Ki kuonekana kama mzaha kwani sherehe yao
itafanyika kwa siku 17 mfululizo, watu wakifurahia kitoweo cha nyama ya ngamia
21 ambao watatiwa visu.
“Diamond Platnumz atamuoa
Zuchu na mpango uliopo ambao nimeamua kuwapa kwa sababu ilitakiwa iwe siri ambayo
nilikuwa nimeificha ni kwamba watachinjwa ngamia 21 kwenye harusi hiyo.”
“Ngamia wataangushwa wa
kutosha, watu wale na sherehe zitakuwa kwa siku 17 mfululizo, kila mkoa
watapata nafasi ya kusherehekea harusi ya Zuchu na Diamond, hivyo tulieni msiwe
na wasiwasi,’ Baba Levo alisema.
Akijibu kuhusu ni kwa nini anahisi Diamond amechukua muda
mrefu kumuoa rasmi Zuchu, Baba Levo alisema;
“Watu hawaoani kwa kukurupuka, watu hawaoani kwa kuigiza. Watu
wanaoana kwa sababu ya mapenzi na mpango uliopangwa.”
Mtunza siri huyo wa Diamond Platnumz alionekana kuipuzilia
mbali harusi ya aliyekuwa ex wa bosi wake, Hamisa Mobetto akisema kuwa hiyo yao
hata haifai kufananishwa hata kidogo na harusi ya msanii wa Nigeria, Davido.
Wikendi iliyopita, Hamisa na Aziz Ki walifunga harusi baada
ya kukamilika kwa taratibu zac ulipaji mahari, shughuli iliyofanyika katika
jiji la kibiashara la Dar es Salaam.
Licha ya sekeseke kuibuka kwamba mwanasoka huyo alilipa
mahari ya ng’ombe 30, mamake Mobetto alikanusha taarifa hizo na kunyoosha
maelezo kwamba Aziz Ki alilipa mahari ya jumloa ya ng’ombe 150 pamoja na kiasi
cha fedha ambacho alisita kukitaja.
Diamond na Zuchu wamekuwa wakisemekana kuwa katika huba zito
tangu mapema 2022 ambapo mara ya kwanza walitania kufunga harusi ilikuwa
kuelekea siku ya wapendanao ya mwaka huo.