
MSANII bora wa Afrika Mashariki mwaka huu kwa mujibu wa tuzo za Trace, Bien Baraza amewapongeza raia wa taifa jirani la Tanzania kwa kuwa watu wenye mapenzi ya hali ya juu kwa wasanii kutoka Kenya.
Akizungumza wikendi iliyopita katika mwendelezo wa mbwembwe
za kusherehekea ushindi wake dhidi ya wababe kama kina Diamond na kuibuka
msanii bora Afrika Mashariki, Bien alisema kwamba kila mara anapokuwa nchini
Tanzania, yeye hujihisi kama vile yuko nyumbani.
Msanii huyo anayezidi kutamba kwa kolabo yake na Marioo
kutoka Tanzania ya Nairobi alisema kwamba watu wa Tanzania wanawapenda wasanii
wa Kenya lakini akatilia mashaka kama mapenzi hayo yanafika hadi kwa Willy
Paul.
“Watanzania wanatusapoti
sana na ukweli ni kwamba wasanii wetu wanapata kuheshimiana kwingineko pia kwa
sababu mara nyingi unapata sisi tunawapenda wengine na hayo mapenzi
yanarudishwa kwetu.”
“Nchini Tanzania sio tu
Bien pekee, kila mtu anapendwa kule isipokuwa Willy Paul,” Bien alisema huku
akitania kwamba kama Watanzania wangependa aishi vizuri nchini mwao basi wampe
mke na nyumba nzuri.
Willy Paul alijizolea idadi kubwa ya maadui mwishoni mwa
mwaka jana alipozua mtafaruku baina yake na baadhi ya wasanii kutoka Tanzania
katika tamasha la Raha Fest.
Pozee aliripotiwa kukejeli kolabo yake na Rayvanny – Mmmh kwa
kuiita ‘takataka’ pindi ilipochezwa akiwa jukwaani kutumbuiza, kisha akaamrisha
itolewe mara moja.
Awali, alikuwa amedaiwa kuzua mtafaruku baina yake na Diamond
Platnumz ambaye alitarajiwa kutumbuiza lakini hakuweza kutumbuiza katika kile
alichokitaja baadae kama ukosefu wa usalama wa kutosha.