

KANISA moja nchini Uganda limeripotiwa kuruka-ruka kwa furaha na vigelegele baada ya mwanasiasa wa upinzani kwa muda mrefu, Kizza Besigye kuripotiwa kuokoka akiwa kuizini.
Mwanasiasa huyo amekuwa kizuizini katika gereza la Luzira
tangu Novemba 2024 baada ya kukamatwa Nairobi na kusafirishwa kinyemela ambapo
anakabiliwa na shtaka la uhaini ambalo adhabu yake ni kifo.
Wachungaji hao ambao walionyesha furaha yao jijini Kampala
Jumapili iliyopita walifurahia ripoti za kuokoka kwa Besigye wakisema kwamba
hiyo ni kazi ya mikono ya Mungu.
"Hivi ndivyo Bwana
anafanya…imeandikwa kwamba hakuna mtu anayeweza kuja kwa mwana isipokuwa baba
amemvuta," alisema Mchungaji Fredrick Ssemazzi wa kanisa la Grace
Assemblies Jumapili.
Taarifa za Besigye kumkubali Yesu kuwa Bwana na Mwokozi wake
ziliibuka kwenye vyombo vya habari mwishoni mwa juma lililopita.
Mmoja kati ya wabunge wa zamani ambaye ni mwandani wa Besigye
anayetambulika kwa jina Mubarak Munyagwa Sserunga alinukuliwa akieleza kuwa
alithibitisha mwenyewe tukio hilo alipokwenda kumjulia hali Dk Besigye huko
Luzira.
Dk Besigye, mgombea Urais mara nne amekuwa gerezani Novemba
mwaka jana.
Anakabiliwa na mashtaka ya uhaini kufuatia kukamatwa kwake na
maafisa wa usalama wa Uganda nchini Kenya.
Awali, alikuwa amezuiliwa katika gereza la kijeshi na kupinga
hatua hiyo kwa kususia chakula hadi kudhoofika kiafya kupelekea mamlaka
kumkimbiza hospitalini.
Hata hivyo, Februari 23 mashtaka yake yalihamishiwa katika
mahakama ya kiraia kama ambavyo mawakili wake walikuwa wanashinikiza.
Baada ya kusomewa mashtaka katika mahakama ya kiraia, Besigye
alighairi mgomo wake dhidi ya mlo japo alizuiliwa tena.
Kesi yake inatarajiwa kuendelea leo hii Ijumaa ya Machi 7
katika mahakama hiyo, huku mawakili wake wakishinikiza kuachiliwa kwa dhamana.