WINNIE Byanyima, mkewe mwanasiasa wa muda mrefu katika siasa za mrengo wa upinzani nchini Uganda amedokeza kwamba hali ya afya ya mumewe ambaye yuko kizuizini inaendelea kuimarika.
Byanyima, ambaye aliwahi kuwa mpenzi wa rais wa sasa Yoweri
Museveni alitoa sasisho hilo kupitia ukurasa wake wa X baada ya kumtembelea
mumewe katika gereza la Luzira anakozuiliwa pamoja na wakili wake Haji Obeid
Lutale.
Katika chapisho hilo, Byanyima alieleza kwamba Kizza Besigye
sasa anaweza kutembea tena na kuzungumza na watu wanaomtembelea gerezani.
“Nilitembelea
@kizzabesigye1 na Haji Obeid Lutale katika Gereza la Luzira leo. Wote wawili
walikuwa na roho nzuri. Nilifarijika kuona @kizzabesigye1 anaweza kutembea na
kuzungumza na wageni wake,” mkewe aliandika.
Pia alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa mahakama kusikiliza
kesi hiyo na kumpa dhamana mumewe, akisema kwamba Besigye amekuwa mtiifu wa
kuhudhuria vikao vya mahakama kwa kesi zake kwa miaka 20 sasa.
“Baada ya miaka 20 ya
kufika mahakamani kwa uaminifu kwa mashtaka mengi ya jinai, HAKUNA sababu ya
kukataa kumpa @kizzabesigye1 dhamana. Jaji lazima asikilize maombi yake na
kukomesha dhuluma hii. Inatosha!” alifoka.
Besigye alikuwa amezuiliwa kizuizini tangu mwaka jana baada
ya kutekwa nyara jijini Nairobi Kenya na kusafirishwa kinyemela hadi nchini
Uganda.
Baada ya mamlaka kukata kuhamisha kesi yake hadi katika
mahakama ya kiraia na kuamua kumfungulia mashtaka katika mahakama ya kijeshi,
mwanasiasa huyo alianza mgomo wa kususia chakula.
Kutokana na hali hiyo, alidhoofika kwa kiasi kikubwa kiasi
kwamba alishindwa kutembea na kuzungumza hadi kupelekwa mahakamani akiwa kwenye
kiti cha magurudumu.
Mnamo Februari 21, Besigye alihamishiwa katika mahakama ya
kiraia na kufunguliwa mashtaka na jinai ambayo adhabu yake ni kifo.
Hakimu alimuru kuzuiliwa kwake hadi Machi 7 wakati kesi yake
inatarajiwa kusikilizwa, hatua ambayo ilimpelekea Besigye kumaliza mgomo wake
dhidi ya chakula.