
KWA mara nyingine, Harmonize amevunja kimya kwa kejeli nyingi dhidi ya jitihada zake za si tu kuzungumza bali pia kuimba kwa lugha ya mkopo – Kiingereza.
Katika chapisho kwenye ukurasa wake wa
Instagram, Harmonize alifichua kwamba amekuwa akiona dharau hizo dhidi ya
Kiingereza chake lakini amekuwa akipuuza, na sasa ni muda wa kuwajibu
wanaokejeli matamshi yake kwa Kiingereza.
Harmonize aliweka wazi kwamba hababaishwi na
wale wanaocheka umahiri wake katika lugha ya Kiingereza, akisema kwamba
ataendelea kukizungumza kwa jinsi anataka mwenyewe.
Aidha, alisema kwamba wale wanaosema
Kiingereza chake ni kibovu, ni kibovu tu kwao lakini kwa yeye mwenyewe na
wengine ambao wanamuelewa, Kiingereza chake mbona kimenyooka tu!
“Sasa acheni niwafanye nyinyi wote
muelewe na tafadhali nifafanulieni, kwa nini nizungumze Kiingereza sahihi? Kwa ajili
ya nani? Kwa nia gani chale wangu?”
“Angalia, Kiingereza changu siku zote
kiwakuwa kibaya kwako na hata sitishiki na hilo hata kidogo,”
alisema.
Msanii huyo alisema kwamba wale wanaodai
hawaelewi anachoimba katika nyimbo zake za Kiingereza wanastahili kujiondoa
kwenye mlolongo na kuwapisha wenye ujumbe umekusudiwa, kwani kama humuelewi
basi ujumbe si wa kwako.
Pia alimaliza kwa kujitapa kwamba yeye ndiye
msanii pekee kutoka Afrika Mashariki nzima anayeimba kwa lugha ya Kiingereza,
kauli ambayo inawatupa baharini wasanii wenzake wanaofanya vizuri kwa miziki ya
Kiingereza kutoka Kenya na Uganda.
“Ukiona hujaelewa ina maana wazo hilo
halikukusudiwa kwako. Mimi ndiye msanii pekee kutoka Afrika Mashariki anayeimba
kwa Kiingereza, chukua hilo!” Harmonize alidai.
Awali, Harmonize alijitetea kwamba yeye ndiye
msanii pekee kutokea Tanzania ambaye wimbo wake umetambulika kimataifa na ambao
uliimbwa kwa 90% Kiingereza.
Bila shaka, hapa alikuwa anarejelea wimbo
wake wa ‘Single Again’ ambao kusema kweli ulikuwa bonge la hit ambayo
iliwavutia watu kadhaa kutoka ndani ya nje ya Afrika.
Akisherehekea mafanikio hayo, Harmonize
alifichua kwamba yeye ana elimu ya darasa la 7 tu na kwamba Kiingereza chote anachokiimba
na kukizungumza hajafunzwa na mtu bali ni kwa juhudi zake binafsi.