
BOSI wa Konde Music Worldwide, Harmonize kwa mara ya kwanza amezungumzia uhusiano wake na Kajala ambao ulivunjika – safari hii akizingatia upande wa mazuri yaliyotokana na uhusiano huo.
Akizungumza na blogu ya Simulizi na
Sauti, Harmonize alibainisha kwamba bado anamheshimu Kajala Masanja kiasi
kwamba anapangac kumpa zawadi nyingine ambayo aliitaja kuwa itampa kumbukumbu
za milele katika kipindi chote cha maisha yake.
Alipobanwa zaidi ikiwa zawadi hiyo
itakuwa jaribio la kumtongoza kumrudia kwa mara ya 3 kama alivyofanya 2022 kwa
kutumia Range Rover, Harmonize alisema itakuwa ni zawadi tu bila kujali ikiwa
atakuwa kwenye ndoa yake au la.
“Nina heshima kubwa sana kwa Kajala
na kwa majaaliwa ya Mwenyezi Mungu, nitamfanyia kitu Fulani kwake ambacho
kitakuwa na kumbukumbu ya milele maishani mwake. Haijalishi kama atakuwa
ameolewa au la, atajua mwenyewe tu,”
Harmonize alisema huku akiachia tabasamu pana.
Alipoulizwa kwa nini safari hii amelegeza
msimamo wake kumhusu mama huyo wa binti mmoja mkubwa – kinyume na alivyomzomea
kwenye wimbo wake wa Dear Ex, Harmonize alisema kwamba alijifunza kuanza
kumheshimu ikizingatiwa kwamba ni mkubwa kwake kiumri.
“Kajala huwa namzungumzia kwa
heshima kwa sababu ananizidi kiumri. Lakini pia ukiachia mbali kigezo hicho,
nikiingia katika mahusiano naye kuna vitu vingi ambavyo nilimsababishia kwa
hasara. Na siwezi lipa hilo kama mwanadamu hata kama sasa hatuko Pamoja ila
bado anastahili heshima yake na hicho ndicho kitu ambacho ninampa,”
Harmonize alisema.
Wawili hao wana historia ndefu ya
mahusiano ya kifaurongo ambayo inarudi nyuma hadi mapema 2021 amapo
walichumbiana kwa muda na kisha kuachana baada ya zogo lililohusisha binti ya
Kajala, Paula, kuchangia.
Hata hivyo, mwaka mmoja baadae mnamo Juni
2022, Harmonize alijitutumua na kumrudisha Kajala kwenye kasri lake la Konde
Village baada ya kumnunulia zawadi ya gari aina ya Range Rover na kuandaa tafrija
kubwa la kumvisha pete ya uchumba Milimani City.
Penzi jipya lilidumu kwa miezi 6 tu kwani
halikuweza kuona mwanga wa mwaka mpya wa 2023, safari hii wakiachana kimya
kimya na siri za kuachana kwao zikafuatia baada ya miezi kadhaa, wote
wakichambana kimafumbo kwenye mitandao ya kijamii.