
MSANII Harmonize amekiri kwamba maombi ya babake ndiyo yanayompa mafanikio yake kimuziki licha ya kwamba baba huyo ndiye alikuwa anapinga sana suala la yeye kuwa mwanamuziki.
Akizungumza na Millard Ayo kwenye Ayo TV, Harmonize Alifichua
kwamba hakumbuki hata siku moja akienda kutafuta huduma kwa mganga katika
maisha yake ya muziki.
Alisema kwamba baba yake ni mtu wa dini sana na ndiye
anayemuombea muda wote tangu ajitose kwenye muziki takribani miaka 10
iliyopita.
“Ninaweza sema hili,
babangu mimi ni mtu wa dini sana. Hata wakati naanza muziki alikuwa ni mtu
ambaye hakuwa kabisa na mimi. Lakini leo hii yeye ni kati ya watu ambao
wananiombea sana,” Harmonize alisema.
“Mimi sikumbuki kama
nishawahi kwenda kwa mganga katika muda wangu wote kama ‘Harmonize’. Hii ni kwa
sababu baba ananiombea sana, ananikumbusha vitu vya msingi,” Harmonize aliongeza.
Msanii huyo alikuwa anazungumzia ufichuzi huu akirejelea kile
alichokigusia kwenye wimbo wake wa ‘Never give up’ kwamba babake alikuwa mtu wa
kuswali sana kiasi kwamba alinunia uamuzi wake wa kuingia kwenye sanaa.
“Acha nikuambie hadithi
Nimezaliwa mtwara
Tanzania
Huko kijijini chitoholi
Hapa mjini nimezamia
Ndoto kucheza boli
Mara ghafla kwa mziki
zikahamia
My dady im sorry swala
tano Hukupenda uliposikia,” moja ya aya kwenye wimbo huo iliimba.
Harmonize pia alifunguka kuhusu picha na video zilizoenea
akipokelewa kwao wakati alipotoka WCB Wasafi ambapo mbuzi alichinjwa na yeye
kupakwa damu.
Alisisitiza kwamba ule haukuwa uchawi wala uganga wowote bali
ilikuwa ni sehemu ya mila za kwao Mtwara ambayo babake alishauri ifanyike.
“Ile ilikuwa ni mila tu
na wazazi wangu, haswa baba alishauri tufanye vile. Hivyo singeweza kukataa na
wala hakuwahi kuniambia kwamba ule ni uchawi wa kumdhuru mtu au tumemwita
mganga aje kufanya mambo yake.”