
SENETA wa kuteuliwa, Karen Nyamu amemtaja marehemu Papa Francis kama mtu ambaye wengi wataukosa uwepo wake si tu katika uongozi wa kanisa Katoliki duniani bali pia katika ushauri na wosia wake kuhusu masuala mbalimbali ya kijamii.
Akizungumza kwenye runinga ya TV47 asubuhi ya Alhamisi, Nyamu
alisema kwamba alivutiwa sana na jinsi Papa Francis alikuwa amejibeba katika
maisha ya kawaida bila kujali tabaka lake.
Kwa mujibu wa Nyamu, Papa Francis alikuwa ni mtu ambaye
alikumbatia waziwazi utandawazi na mitandao ya kijamii japo pia alionya kuhusu
teknolojia ya AI na madhara yake.
“Nilimpenda Papa Francis
kwa sababu alikumbatia mitandao ya kijamii na akaonya dhidi ya teknolojia ya AI
akisema kwamba teknolojia kupita kiasi ni hatari kwa moyo.”
“Papa alikuwa mtu wa
kawaida, alionekana kukwepa kabisa maisha ya kifahari na kuchagua maisha ya
kawaida tu na kusema kweli tunaenda kukosa ushawishi aliokuwa nao kote duniani
na tunatumai Papa mpya atachukua kutoka kwa Francis na pia atakuwa na athari
sawia ulimwenguni kote,” Nyamu alisema.
Kuhusu uwezekano wa Papa mpya kutoka bara la Afrika kwa mara
ya kwanza katika historia, Nyamu alisema kwamba ni jambo ambalo kila mtu
anatumai litafanyika hivyo, akidai kwamba bara la Afrika sasa liko mbele katika
kila sekta.
“Papa Mwafrika litakuwa
jambo la kufurahisha sana kwa dunia kwa sababu Afrika sasa hivi ndio kifua
mbele katika kila sekta,” Nyamu alisema.
Nyamu pia alimtaja Papa Francis kama kiongozi ambaye hakuwa
anapenda mivutano ya kisiasa, akirejelea jinsi alivyozungumzia suala la Urusi
kuishambulia Ukraine.
“Namkumbuka Papa Francis
kama mtu aliyekuwa papa huria ambaye hakutaka kuegemea upande wowote. Hakuogopa
kuzungumzia kuhusu vita vya Urusi na Ukraine lakini pia Israel na Gaza.”
“Nakumbuka wakati mmoja
alivutia ukosoaji kwa kusema kwamba Urusi ilichochewa na muungano wa NATO
kuishambulia Ukraine na kukwepa kumtaja Vladmir Putin moja kwa moja kama
mchokozi,” Nyamu alimkumbuka.
Papa Francis alifariki Jumatatu wiki hii na anatarajiwa
kuzikwa Jumamosi.