
MBUNGE wa bunge la jumuiya ya Afrika Mashariki, EALA, David Ole Sankok amevutia maoni mseto baada ya kudai kwamba aliyekuwa mgombea wa uenyekiti wa AUC, Raila Odinga anastahili kukabidhiwa wadhifa katika bunge la kitaifa Kenya.
Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Ole Sankok alitoa ombi
lisilo la kawaida kwa wabunge kutafuta njia ya kumbandua mamlakani mwanasiasa
mmoja ili kumtengenezea Odinga nafasi ya wadhifa.
Sankok alisema kwamba wakati umefika wa Odinga kuvishwa taji
akimtaja kama simba wa bara zima la Afrika.
“Bunge la Kenya linafaa
kumbandua mtu ili kuunda nafasi ya Simba wa Afrika, Mfalme asiye na taji ~ Baba
Raila Odinga. Tumuweke taji sasa,” Ole Sankok alisema.
Mwanasiasa huyo aliendeleza kutoa wito huo kwa wabunge
akisema kwamba Odinga anaweza tengenezewa nafasi bungeni ya ama kuwa kiongozi
wa wengi bungeni au spika.
“Tunaweza kuunda nafasi
ya Waziri Mkuu au kutafuta fomula ya Raila Odinga kuteuliwa bungeni kuchukua
wadhifa wa kiongozi au Spika wa wengi au tukabiliane na Tsunami,” alisema.
Kabla ya uchaguzi wa AUC uliofanyika jijini Addis Ababa,
Ethiopia Jumamosi iliyopita, Ole Sankok alisema kwamba ilikuwa ni lazima kwa
Odinga kushinda uchaguzi huo la sivyo angelitifua vumbi la siasa nchini baada
ya kushindwa.
“Raila Odinga lazima
ashinde uenyekiti wa AUC kwa sababu kushindwa kutakuwa kurusha roketi
kumpandisha kwenye siasa za ndani kama Bomu la nyuklia,” alisema.
Hata hivyo, Odinga alikosa bahati ya kuibuka mshindi baada ya
kujiondoa katika raundi ya 6 ya kinyang’anyiro hicho kikali.
Mgombea kutoka Djibout Mahmoud Ali Youssouf aliibuka mshindi
baada ya kupata thuluthi mbili ya kura hitajika ya 33 na kumrithi mwenyekiti
anayeondoka Moussa Faki.
Baada ya Odinga kubuma kwenye uchaguzi wa AUC, sasa
inasubiriwa kuonekana ni mkondo upi wa kisiasa atakaochukua baada ya kurejea
humu nchini wiki hii.