
RAIS William Ruto amedai kwamba hatua ya kiongozi wa ODM, Raila Odinga kuwania uenyekiti wa AUC, japo bila mafanikio, iliwaunganisha Wakenya wote pamoja.
Akizungumza katika ikulu ya Mombasa alikomkaribisha Odinga
aliyerejea nchini baada ya kupoteza kinyang’anyiro cha AUC wiki iliyopita, Ruto
alimshukuru kwa kuliwakilisha taifa katika ngazi za kimataifa.
“Ninajivunia kwamba Raila
Odinga aliweka juhudi zote kuwa mwaniaji mwenye nguvu barani Afrika. Alifanya
safari angani na barabarani akizuru mataifa mbalimbali kujipigia debe si tu kwa
niaba yake bali pia kwa niaba ya Kenya,’ Ruto alisema.
“Uwaniaji wake uliwaleta
pamoja Wakenya wote. Nafikiri uwaniaji wake ulivutia sapoti kutoka kwa mirengo
yote ya kisiasa – watu kutoka serikali, upinzani na kila mtu. Tuliungana nyuma
ya uwaniaji wa Raila Odinga kama mwenyekiti wa AUC,” rais aliongeza.
Mkuu wa taifa alichukua fursa hiyo kuwashukuru wote
waliochangia kwa njia kubwa ama ndogo katika kutangaza azma ya Odinga katika
kinyang’anyiro cha AUC.
Rais pia aliwashukuru wakuu wa mataifa 22 ambao walisimama imara
ya mwaniaji wa Kenya katika raundi zote hadi alipojiondoa kunako raundi ya 6.
“Ningependa kuwashukuru
ndugu zangu na marafiki zangu kote barani Afrika kwa ishara yao ya mshikamano
na sapoti ambayo walionyesha kwa Kenya na kwa Raila Odinga ambaye alikuwa
mgombea wetu.”
Raila Odinga alijiondoa katika raundi ya 6 baada ya kupata
kura 22 dhidi ya kura 26 alizopata mshindani wake kutoka Djibout, Youssouf
Mahmoud Ali.Youssouf hatimaye aliibuka mshindi katika raundi ya 7 ambapo
alipata akidi hitajika ya kura 33 na kuchukua uongozi kutoka kwa Moussa Faki
aliyekuwa anamaliza hatamu yake.