
MAAFISA wa polisi katika kaunti ndogo ya Kikuyu asubuhi ya Jumatano walivamia shamba lenye ukubwa wa takribani nusu ekari ambalo ni la kukuza bangi.
Katika video zilizochukuliwa kutoka eneo hilo la Kidfarmaco,
polisi kwa ushirikiano na machifu wa eneo hilo walitaarifiwa kuhusu shamba hilo
ambalo limekuwa likikuza dawa za kulevya aina ya bangi kisiri kwa muda mrefu.
“Asubuhi tumepata ripoti
kwamba mwenye hili shamba ambaye anapanda bangi. Tumepata ujumbe kwamba kando
na kupanda mahindi, huku ndani kuna mimea ya bangi. Na hata mkiona hapa karibu
amefanya unyunyiziaji ili kuhakikisha kwamba bangi inanawiri,” chifu alisema.
Kwa mujibu wa taarifa, shamba hilo linamilikiwa na raia wa
Burundi 3 ambao hata hivyo hawakuweza kutiwa mbaroni wakati wa uvamizi huo wa
vyombo vya dola.
Walisema kwamba Warundi hao walikuwa wanafanya ukulima wa
mahindi katikac sehemu ya mbele ya shamba hilo huku kwenda ndani wakifanya
ukulima haramu wa bangi.
“Kazi kibarua tuko nayo
ni kumtafuta mwenye hili shamba na wale ambao wameajiriwa kufanya kazi hapa. Eneo
la shamba ni kama nusu ekari na tunajua tunatafuta washukiwa wawili na bila
shaka mwenye shamba,” chifu alisema.
Chifu huyo alitoa wito kwa wamiliki wa mashamba ambayo
hayatumiki kuanzisha miradi halali katika mashamba hayo ili kuzuia visa vya
ukuzaji wa dawa haramu za kulevya.
Pia alitoa wito kwa majirani kuwa macho ili kuhakikisha
wenzao wanafanya shughuli halali katika vipande vyao vya ardhi, akisema kwamba
ikiwa majirani wa shamba hilo wangekuwa makini, basi wangegundua kwamba mwenzao
anafanya kilimo cha bangi na kupiga ripoti mapema.