
MBUNGE wa Kapseret Oscar Sudi kwa mara ya kwanza amezungumzia Kauli zinazozunguka kitembo chake cha kielimu.
Akizungumza Jumapili katika Eneobunge la Kiambaa, Sudi
alikiri waziwazi kwamba wanaosema hajasoma wanasema ukweli, huku akijitetea
kwamba hakuna mahali amewahi simama na kupingana na Kauli hiyo.
Hata hivyo, Sudi alijipiga kifua kwamba licha ya kuambiwa
hajasoma, katika Eneobunge lake amepanga masuala ya maendeleo hata kuwashinda
wale wanaojidai kuwa wasomi.
“Mimi niwaulize nyinyi, si
mnasikia wanasema mimi sikuenda shule? Mnafikiri hao watu wanasema uongo? Mmewahi
sikia mahali nikisema nilienda shule? Lakini ukikuja huko kwangu nimepanga
maneno rafiki yangu kwa sababu ya ukarabati,” Sudi alisema.
Sudi alisema kwamba watu wachache tu ndio wamesema humu
nchini huku akidai kwamba sasa hivi hata akisimama urais anaangusha wengi
wanaojidai kuwa wasomi.
“Hata nikisimama urais si
naangusha hawa? Sisi watu wa hoe hae ndio wengi,” Oscar Sudi aliongeza.
Mwezi Februari, Sudi alipapurana kwenye mitandao wa X na
seneta wa Nairobi, Edwin Sifuna wakati seneta huyo alipomkashifu Ruto kwa
kujihusisha na watu wasio na elimu akimtolea mfano mbunge huyo ambaye ni
mwandani wa rais.
“Ruto alituambia kwamba ana PhD, mimi sijawahi ona mtu wa
PhD anayetembea na mtu aliyeachia shule darasa la pili. Inawezekana aje wewe
una PhD na unatembea na Sudi. Inawezekana aje hiyo kuwa ukweli,” Sifuna alisema katika mahojiano na runinga
ya Citizen TV.
Hata hivyo, Sudi alimfokea Sifuna akimwambia kwamba yeye hana
hata robo ya ujuzi wake, kando na kitembo cha masomo.
“Sifuna
unaweza jilinganisha na mimi? Unajua IQ yangu na yako hazilingani hata kwa
robo. Tafuta mtu mwingine ambaye unaweza jilinganisha naye au mwenye
utalinganisha na Ruto,” Sudi alimwambia.
“Mimi niko katika kiwango changu na sio kwamba
ninaringa au nini lakini unaweza ulizia kuhusu historia yangu. Huna hata robo
ya ujuzi wangu. Kwa hivyo usikuwe mpuuzi kuongea kama mtoto,” Sudi aliongeza.
Sudi alisema kwamba Sifuna amekuwa na hulka ya kushambulia
kila mtu akidhani ni haki yake, lakini kwake amefika kwenye mwamba.