
NAIBU wa rais aliyebanduliwa, Rigathi Gachagua amelilia vyombo vya usalama akisema maisha yake yamo hatarini.
Kupitia taarifa rasmi aliyoichapisha kwenye kurasa zake
katika mitandao ya kijamii, Gachagua aliandikia wakuu wa vitengo mbalimbali vya
usalama akiwemo IG wa polisi Douglas Kanja, na kudai kwamba amepokea vitisho
kuhusu maisha yake.
Gachagua alitolea mifano mashambulizi ambayo alidai yamekuwa
yakilenga mikutano yake ya kisiasa na kudai kwamba ipo njama fiche ya kulenga
maisha yake.
“Kama unavyojua, una wajibu
wa kikatiba kulinda kila mkenya na mali zao kama ilivyoainishwa katika katiba
ya 2010. Hata hivyo, katika kesi hii, bwana Kanja unaendeleza mashambulizi na
uhalifu,” sehemu ya barua hiyo iliyoelekezwa kwa ofisi ya IG Kanja
ilisoma.
Aidha, Gachagua alilalamikia kuondolewa kwa walinzi wake
akisema kwamba suala hilo limemuanika bayana kwa mashambulizi ambayo sasa
yameweka maisha yake hatarini.
“Uliondoa walinzi wangu
katika njama iliyopangwa vizuri ili kunianika zaidi kwa visa vya kushambuliwa
na vijana kwa kushirikiana na vyombo vya usalama,” alilalama zaidi akitolea
mifano ya mashambulizi dhidi yake katika hafla mbalimbali za umma.
Kisa cha hivi punde cha mashambulizi dhidi ya naibu wa rais
huyo wa zamani kilijiri wiki mbili zilizopita katika hafla ya ibada kanisani
PCEA Mwiki.
Iliwabidi walinzi wake wa Kibinafsi kuingilia kati na
kufyatua risasi hewani ili kutawanya kundi la vijana ambao walifika katika
kanisa hilo wakipiga kelele kuhusu Gachagua.
Gachagua amekuwa mkosoaji mkuu wa serikali ambayo kwa kipindi
kimoja alikuwa anaitetea kwa jino na ukucha hadi pale alipobanduliwa ofisini
mnamo Oktoba 2024.