
WAKAAZI wa Kijiji cha Kamagut katika kaunti ya Uasin Gishu walipigwa na butwaa wikendi iliyopita baada ya vijana wa boma moja kufukua mwili wa marehemu baba yao aliyezikwa miaka 15 iliyopita wakimtaka aingilie kati mzozo wa shamba.
Kwa mujibu wa The Standard, mwili wa mzee
huyo ulikuwa umefukuliwa na watoto wake, ambao walidai ni yeye pekee anayeweza
kuwatetea dhidi ya vitisho vya mara kwa mara na mtu anayedai umiliki wa shamba
lao la ekari 17, linalodaiwa kurithi kutoka kwa nyanya yao.
Ripoti hiyo ilieleza kwamba Watoto wa
mzee huyo walifikia uamuzi huo baada ya majambazi kuendelea kuwatishia
kuwaondoa kwenye mali hiyo tangu mwaka 2022.
Walieleza kuwa walitoa taarifa za vitisho
hivyo kwa mamlaka, lakini bila msaada wowote, walimgeukia mtu huyo ambaye
alikuwa akiwalinda wakati wote akiwa hai.
Mtoto mmoja wa marehemu, alisema
unyanyasaji huo uliongezeka siku ya Jumamosi wakati vijana waliokuwa na mapanga
walipovamia shamba hilo na kuanza kupanda mazao sehemu moja.
Alisema yeye na ndugu zake kwa heshima
waliwaomba wavamizi hao kuondoka kwenye mali hiyo, lakini walishambuliwa kwa
mapanga na visu.
Hata hivyo, polisi walifika katika boma
hilo na kuwatia mbaroni vijana hao 3 pamoja na mama yao mjane kwa kile walisema
kwamba ni kuzua usumbufu kwa marehemu.
Kamanda wa polisi kaunti ya Uasin Gishu
Benjamin Mwanthi alithibitisha kwa The Standard kuwa wanne hao walikamatwa kwa
kufukua mwili bila agizo la mahakama.
"Ni kinyume cha sheria kufukua maiti
iliyozikwa-hata ikiwa ni ya jamaa-bila idhini inayofaa. Pia ni kinyume cha
sheria kuingilia mabaki ya binadamu," alisema Kamanda wa Kaunti.