
Kwenye PATANISHO ya Radio Jambo na watangazaji Gidi na Ghost, mwanamume mmoja kwa jina Clarkson Wamae mwenye umri wa miaka 29 aliomba kupatanishwa na mkewe Fridah mwenye umri wa miaka 26.
Kwa mujibu wa Wamae, alioana na Frida miaka miwili iliyopita
akiwa na watoto wawili kabla ya kubarikiwa na mtoto mwingine pamoja.
Hata hivyo, miezi mitatu iliyopita, Fridah aliondoka
nyumbani ghafla na wale watoto 2 aliokuja nao katika ndoa na kumuacha yule
mdogo aliyezaa katika ndoa na Wamae, akiwa na umri wa mwaka mmoja na nusu.
Wamae aliomba kupatanishwa naye ili arudi kumlea mtoto mdogo
ambaye yuko chini ya malezi ya mamake ambaye Wamae alisema ni mdhaifu kutokana
na ugonjwa.
“Nilikuwa nimetoka nyumbani
kwenda kazini mwaka jana Novemba. Nilimuoa na nilimpata na watoto 2 tukaja
tukafanikiwa tukapata mtoto mmoja alimuacha kwa mamangu na mama ni mdhaifu
hajiwezi, nilikuwa naomba tuongee tusemezane arudi…”
“Wameniambia ako Kakamega, nikijaribu kumtafuta simu inaingia lakini
hachukui. Nikiondoka nilikuwa natuma hela za matumizi kila baada ya mwezi. Aliacha
mtoto mdogo wa mwaka na nusu mwenye nimezaa na yeye, wale wengine wako kwao na
sasa mdosi wangu nimeongea na yeye ako tayari kuwasaidia watoto hao wakuje
penye mimi nafanya kazi,” Wamae alisema.
Kwa upande wake, Fridah alipopigiwa simu, hakuweza
kupatikana kwa simu jambo ambalo lilikwamiza azma ya Wamae kutaka kurudiana na
mtoto wake.
Wamae alihisi huenda mkewe alizima simu baada ya kusikiliza
redio, akifichua kwamba ni shabiki mkubwa wa Radio Jambo, haswa Patanisho.
Baada ya kubanwa na Gidi kuhusu chanzo cha mkewe kuondoka,
Wamae alikiri kwamba walikosana kwa nyumba na akamzaba kofi, japo alisema
hakuwahi kurudia kumpiga tena.
“Fridah kama uko mahali unanisikiliza mimi bwanako Wamae, naomba
ukanisamehe nilikukosea. Urudi kwa nyumba yako. Nakuomba kama kuna kitu ambacho
unahitaji unaniambia kama bwanako nitakusaidia kwa sababu hapa kazini
wameniambia wataniongeza kitu,” Wamae alimaliza.