Mwanawe mwanahabari marehemu Catherine Kasavuli avunja kimya kufuatia kifo chake

Martin amewashukuru wote ambao wamekuwa wakisaidia familia yao kwa njia moja au nyingine.

Muhtasari

Mwanawe Kasavuli amewashukuru wote ambao wamekuwa wakisaidia familia yao kwa njia moja au nyingine kufuatia kifo cha mama yake.

•Martin amefichua kuwa marehemu mama yake aliacha salio la bili ya hospitali ya hadi Ksh 4 milioni wakati alipofariki.

Mtangazaji Catherine Kasavuli
Image: HISANI

Mtoto wa pekee wa mtangazaji mkongwe Catherine Kasavuli ambaye aliaga dunia mwishoni mwa mwezi uliopita amewashukuru wote ambao wamekuwa wakisaidia familia yao kwa njia moja au nyingine kufuatia kifo cha mama yake.

Bi Catherine ambaye sura yake ilikuwa maarufu sana kwenye runinga za Kenya alifariki mnamo Desemba 29, 2022 katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta ambapo alikuwa amelazwa baada ya kugunduliwa na saratani ya shingo ya kizazi.

Martin Kasavuli ametumia ukurasa wa Instagram wa marehemu mama yake kutoa shukrani za dhati kwa Wakenya ambao wamekuwa wakitoa msaada wa aina mbalimbali kwa familia yao tangu mamake mpendwa alipoaga dunia.

Wakati huo huo, amefichua kuwa marehemu mama yake aliacha salio la bili ya hospitali ya hadi Ksh 4 milioni wakati alipofariki.

"Tumepokea jumbe nyingi sana hasa kutoka kwa marafiki na familia kutoka kwa watu wanaoishi nje ya nchi wakiuliza jinsi wanaweza kuchangia bili inayosubiriwa ya Ksh 4 milioni," aliandika kwenye Instastori za akaunti ya mamake.

"Naomba wasiliana nami kupitia DM au ujibu Instastory hii nitakutumia namba ya  (mjomba yangu, kaka na Catherine) Unaweza kutuma mchango wako. Mungu akubariki." alisema.

Bi Catherine Kasavuli alifariki akiwa na umri wa miaka 60  takriban wiki moja iliyopita baada ya kupambana na saratani kwa muda.

Mwajiri wake, KBC alithibitisha kifo hicho.

"Mtangazaji nguli, Catherine Kasavuli, amefariki. Aliaga dunia Alhamisi usiku (Desemba 29) katika KNH alikokuwa akipokea matibabu," KBC ilitangaza.

Kasavuli alikuwa amelazwa katika kituo hicho tangu Oktoba 26. Mfanyakazi mwenzake katika KBC alikuwa amewaarifu Wakenya kuhusu hali yake.

Kabla ya kukumbana na kifo chake, Kasavuli alikuwa amerejea kwenye runinga baada ya KBC kumwajiri miongoni mwa wanahabari wengine wakongwe ili kuboresha kituo hicho cha habari.

Marehemui alikuwa amechukua mapumziko ya miezi minne na kurudi kwenye umme kupitia Instagram mwezi Oktoba.

Mnamo Novemba, wafanyakazi wenzake na marafiki katika tasnia ya habari walihamasisha watu kuchangia damu kwa ajili ya kutiwa damu mishipani baada ya kulazwa katika hospitali kuu ya KNH.