Bw na Bi Pozee! Willy Paul aaga ukapera huku mapenzi na Miss P yakipamba moto

Pozee amethibitisha kwamba hajamsamehe tu mrembo huyo bali pia sasa wao ni wapenzi.

Muhtasari

•Willy Paul amethibitisha kufufuka kwa mahusiano yake na msanii wake katika Saldido International, Miss P.

•Pozee alionyesha video yao wakifurahia muda pamoja ndani ya gari kwenye barabara ya Express Way, jijini Nairobi.

Willy Paul na Miss P
Image: INSTAGRAM// WILLY PAUL

Mwimbaji Wilson Radido almaarufu Willy Paul amethibitisha kufufuka kwa mahusiano yake na msanii wake katika Saldido International, Miss P.

Wawili hao ambao walizika tofauti zao siku chache zilizopita baada ya Miss P kuchukua hatua ya kijasiri na kumuomba msamaha bosi huyo wake.

Willy Paul, almaarufu Pozee sasa amethibitisha kwamba hajamsamehe tu mrembo huyo bali pia sasa wao ni wapenzi.

"Ni jambo la mapenzi. Bwana na Bibi Pozee. Yaani  P's" Willy Paul alisema kwenye mtandao wa Instagram siku ya Jumapili.

Mwimbaji huyo wa zamani wa nyimbo za injili aliambatanisha ujumbe wake na picha yake nzuri na msanii huyo wake.

Pia alionyesha video yao wakifurahia muda pamoja ndani ya gari kwenye barabara ya Express Way, jijini Nairobi.

"Mwanaume sio single. Niko out na mpenzi," alisema kwenye video hiyo.

Siku ya Ijumaa, mwimbaji huyo wa nyimbo za mapenzi alichapisha picha nzuri yake na Miss P na kuonyesha upendo mkubwa kwa malkia huyo.

"Unashika ni kama unaimiliki kwa sababu unaimiliki!" Pozee aliandika chini ya picha iliyomuonyesha akishika kiuno cha Miss P.

Mwimbaji huyo wa zamani wa nyimbo za injili pia alichapisha picha yake nyingine na kipusa huyo na kukiri kumpenda.

"Nakupenda" aliandika.

Watumiaji wengi wa mtandao waliwapongeza wasanii hao wawili kwa kurekebisha uhusiano wao huku baadhi yao wakionekana kushangazwa na jinsi mambo yalivyoenda kasi katika kipindi cha wiki moja iliyopita.

Safari ya kurejesha uhusiano mzuri kati ya wawili hao ilianza mapema wiki jana baada ya Miss P kumuomba msamaha bosi huyo wake katika Saldido  kwa kumchafulia jina kwa madai mazito takriban miaka miwili iliyopita.

Hivi majuzi, Miss P akizungumza na Nicholas Kioko aliomba msamaha kwa Willy Paul kwa mambo yote aliyosema kumhusu.

"Willy Paul unajua tulikuwa na historia, yametokea mambo mengi ambayo sisi sote hatujivunii. Ni miaka miwili imepita na si vizuri kuelendelea kubebeana chuki kwa sababu inachosha,” Malkia huyo alisema.

Miss P alitaja msukumo wa nafsi yake kama sababu kuu ya kumchafulia jina Willy Paul takriban miaka miwili iliyopita.

"Ukiona hivyo nitajaribu kukutafuta lakini ukiona unaweza kufikia kabla sijafanya"

Aidha, alibainisha kwamba anajuta kuzungumza vibaya kuhusu Willy Paul wakati wa mahojiano ambayo alifanya awali