Fahamu kwa nini mkataba wa Stevo Simple Boy ulisitishwa

MIB ilisema kuwa uamuzi wa kusitisha mkataba huo ulifuatia mkutano wa siku mbili wa wanachama.

Muhtasari

•MIB ilithibitisha kuwa sasa wameingia katika kipindi cha siku 35 cha ubadilishaji wa usimamizi wa rapa huyo kutoka Kibera.

•MIB ilisema uamuzi huo ufuatia tuhuma nzito zilizotolewa dhidi ya kampuni hiyo na mke wa Stevo Simple Boy, Grace Atieno

Mwanamuziki Stivo Simple Boy
Image: HISANI

Kampuni ya Men in Business Management (MIB) imeeleza zaidi kuhusu kukatishwa kwa mkataba wake na mwimbaji Stephen Otieno Adera almaarufu Stevo Simple Boy.

Katika mahojiano na mwandishi Samuel Maina, MIB ilithibitisha kuwa sasa wameingia katika kipindi cha siku 35 cha ubadilishaji wa usimamizi wa rapa huyo kutoka Kibera.

MIB ilisema kuwa uamuzi wa kusitisha mkataba huo ulifuatia mkutano wa siku mbili wa wanachama.

“Kufuatia tuhuma zisizo sahihi na zisizo halali, na uongo mwingi ambao umetolewa ambao umeharibu sifa ya kampuni, ndiyo maana timu nzima imekaa na kutoa uamuzi kwamba tutoke nje ya mkataba. ,” mwakilishi wa MIB alisema.

Aliongeza, "Tutafuata taratibu halali kwa njia sahihi ambayo ingeweza kufuatwa tangu mwanzo. Mchakato tutakaouchukua ni wa halali na wa haki kwa mpito huo kufanyika ndani ya siku 35.”

MIB ilisema maamuzi kati ya wanachama yalianza mwishoni mwa wiki iliyopita kufuatia tuhuma nzito zilizotolewa dhidi ya kampuni hiyo na mke wa Stevo Simple Boy, Grace Atieno.

"Kila mtu alifikia hitimisho la mwisho. Sio kwa sababu ya madai, na hatutaki kujilinda kwa njia yoyote. Tunataka tu kumwacha msanii huru kwa mustakabali mwema pia. Madai hayo yanatia wasiwasi,” Kampuni ilisema.

Wasimamizi hao walifichua kuwa walikaa chini na Stevo siku moja baada ya madai hayo kupeperushwa kwenye vlogu maarufu ya YouTube.

Walisema kuwa wakati wa kikao chao na msanii huyo, alibainisha mwenyewe kwamba kampuni hiyo imekuwa ikimsaidia kila wakati na akadai kuwa anashinikizwa kwenda dhidi yao.

“Tulimpa ushauri. Tulimwambia kwamba uamuzi wowote utakaotoka kwa upande wetu anapaswa kuuchukua vyema na uamuzi wowote utakaotoka upande wake pia tutauchukua vyema,” MIB alisema.

MIB iliweka wazi kuwa uwezekano wa kurudiana na rapa huyo wa Kibera ni mdogo sana kwani athari ya jumla ya madai yaliyoibuliwa ni ya kutia wasiwasi mkubwa.

Mkataba wa Stevo Simple Boy na Men In Business ulikatizwa rasmi Jumatatu, Juni 26, siku mbili tu baada ya mkewe kudai kuwa msanii huyo anatatizika kifedha na kwamba usimamizi umekuwa ukimnyanyasa.