Hisia zamzidia Akothee baada ya mwanafunzi kuhatarisha maisha, kuruka katika boma lake kuomba karo

Pia alizungumza na mwanafunzi huyo wa shule ya upili kuhusu talanta yake ya muziki na kumtia moyo kuendelea kuisukuma.

Muhtasari

•"Soma kwa bidii… Msalimie mama yako," Akothee alisikika akimwambia mwanafunzi huyo baada ya kumpa mlezi wake karo.

•Aliguswa na jinsi ambavyo mvulana huyo ambaye alikuwa amevalia sare alivyohatarisha maisha yake ilitu  kumfikia na kumuomba karo ya shule.

Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Mwanafunzi mmoja wa shule ya upili aliruka ndani ya boma la mwimbaji Akothee katika eneo la Rongo, Kaunti ya Siaya siku ya Ijumaa katika azma ya kuomba karo ya shule.

Mwanamuziki na mjasiriamali huyo alishiriki video ya moja kwa moja iliyomuonyesha akiwa katika mazungumzo na mvulana huyo na mlezi wake ambapo walizungumza kwa Lugha ya Dholuo.

Katika video hiyo iliyochapishwa kwenye ukurasa wake wa Facebook, mama huyo wa watoto watano alionekana akimkabidhi mlezi wa mvulana huyo hundi na kiaso cha pesa kisichobainishwa kabla ya kumwagiza amletee risiti baada ya kukamilisha malipo ya karo ya shule.

"Soma kwa bidii… Msalimie mama yako," Akothee alisikika akimwambia mwanafunzi huyo baada ya kumpa mlezi wake karo.

Pia alisikika akizungumza na mwanafunzi huyo wa shule ya upili kuhusu talanta yake ya muziki na kumtia moyo kuendelea kuisukuma.

Mwimbaji huyo hakuweza kuficha alivyoguswa na jinsi ambavyo mvulana huyo ambaye alikuwa amevalia sare yake ya shule alivyohatarisha maisha yake ilitu  kumfikia na kumuomba karo ya shule.

"Mvulana huyu alihatarisha maisha yake na kuruka ndani ya boma langu kwa ajili ya karo ya shule," Akothee alisema na kuambatanisha ujumbe wake na emoji za uso wenye machozi,  kueleza jinsi kitendo cha mvulana huyo kilivyomfanya awezwe na hisia.

Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Mbali na muziki na biashara, mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 43 pia anajulikana kwa kazi zake za hisani na hapo awali amewahi kuwasaidia wazazi wengi wanaotatizika kuwasomesha watoto wao. Matendo yake yamethibitisha kuwa ana thamani kubwa katika elimu na pia moyo mzuri wa kusaidia.

Mwishoni mwa mwezi uliopita, alifichua kwamba pia amewahi kuwasaidia wanafamilia wake wote kwa njia moja au nyingine ingawa baada ya yote, wengi wao walimtema na kuamua kutosimama naye.

Nimesaidia familia yangu.Nilipopata umaarufu, familia yangu haikuwahi kujua mahali nilipokuwa na nilichokuwa nikifanya. Baada ya hapo niliwasaidia wote. Nikichapisha taarifa zangu za benki leo, mtagundua wanafamilia wangu wote wametabasamu hadi benki,” Akothee alisema.

Pia amewasomesha mabinti zake wote hadi chuo kikuu huku binti wake wa tatu, Fancy Makadia akiwa wa mwisho kuhitimu mapema mwaka huu. Wanawe wawili wadogo bado wanasoma nchini Ufaransa ambako wanaishi na baba ya mtoto wake wa mwisho.