Eric Omondi apeleka vyakula kwa mwandamanaji aliyekamatwa na polisi aliyejifanya mwanahabari

Victor alikamatwa alipokuwa akilalamika baada ya maafisa wa polisi kudaiwa kumrushia mtoto wake vitoa machozi

Muhtasari

•Eric Omondi alitembelea kituo cha polisi ambako Victor anazuiliwa, akamjulia hali na kumpatia vyakula vikiwemo mkate, maziwa na soda.

•Eric pia alielezea kusikitishwa kwake na walinda sheria kwa kutomwasilisha mwandamanaji huyo mahakamani siku ya Alhamisi.

Image: INSTAGRAM// ERIC OMONDI

Alhamisi, mchekeshaji maarufu Eric Omondi alimtembelea Bw Victor Juma ambaye alikamatwa kwa njia isiyo ya kawaida siku ya Jumatano na afisa wa polisi aliyekuwa amevalia nguo za kawaida ambaye alijifanya mwandishi wa habari ili kuwakamata waandamanaji katika eneo la Mathare, Kaunti ya Nairobi.

Katika tukio lililonaswa kwenye kamera na vyombo mbalimbali vya habari, mwandamanaji Victor Juma ambaye alikuwa akilalamika baada ya maafisa wa polisi kudaiwa kumrushia mtoto wake vitoa machozi wakati wa maandamano ya kupinga serikali siku ya Jumatano alionekana akikamatwa na afisa mmoja ambaye alimvizia kwa kujifanya kurekodi maandamano hayo kwenye kamera.

Siku ya Alhamisi, mchekeshaji Eric Omondi alitembelea kituo cha polisi ambako Victor anazuiliwa, akamjulia hali na kumpatia vyakula vikiwemo mkate, maziwa na soda.

Katika video aliyochapisha Eric kwenye ukurasa wake wa Instagram, mchekeshaji huyo alionekana akishiriki mazungumzo na Juma ambaye alimpa maelezo ya jinsi alivyokuwa akiendelea ndani ya seli.

"Tumepata Juma, tutaenda kumtetea huko," Eric Omondi alisema.

Victor Juma ambaye alionekana kufurahishwa na ziara hiyo alimshukuru mchekeshaji huyo kwa kumjulia hali na kumpatia chakula.

Eric pia alielezea kusikitishwa kwake na walinda sheria kwa kutomwasilisha mwandamanaji huyo mahakamani siku ya Alhamisi.

Hakufikishwa mahakamani, si ni HARAMU??? Unawezaje kuwekwa saa 48 kwenye seli za polisi,” alisema mchekeshaji huyo.

Tukio la kukamatwa kwa Juma siku ya Jumatano lilirekodiwa kwenye kamera na vyombo mbalimbali vya habari na video za tukio hilo zimekuwa zikivuma kwenye mitandao ya kijamii na kuzua hisia tofauti kutoka kwa wanamitandao.

Jumatano jioni, Baraza la kusimamia Vyombo vya Habari nchini (MCK) liliwakosoa maafisa wa polisi kwa kujifanya wanahabari wakati wa maandamano yanayoendelea ya kupinga serikali.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari, Mkurugenzi Mtendaji wa MCK David Owoyo alibainisha kuwa kitendo cha polisi kujifanya waandishi wa habari ili kuwakamata waandamanaji wakati wa maandamano yanayoongozwa na viongozi wa Azimio la Umoja ni tishio kwa kazi ya waandishi wa habari.

"Baraza la Vyombo vya Habari nchini Kenya limegundua kwa wasiwasi mkubwa visa vya maafisa wa usalama kujificha kama wanahabari wanaoripoti maandamano kwa nia ya kuwakamata waandamanaji," taarifa ya MCK ilisoma.

"Uigizaji wa waandishi wa habari na polisi ni utovu wa maadili ya kazi kwa upande wa polisi na unahatarisha maisha ya waandishi wa habari wakiwa kazini."

MCK ilibainisha kuwa wanahabari wanalindwa chini ya vifungu vya 33, 34 na 35 vya katiba na kuwataka polisi kuheshimu haki za wanahabari.