Diamond hatimaye aeleza sababu ya kuzozana, kutupiana vijembe hadharani na Alikiba

Wakati huohuo, Diamond alionekana kumkubali mpinzani wake Alikiba na kubainisha kuwa nyimbo zake pia ni nzuri.

Muhtasari

•Diamond alifichua kuwa matusi ya hadharani na wasanii wenzake k.v Alikiba yana lengo la kusisimua tasnia ya muziki wa bongo.

•“Pongezi kwa kila mtu, kila mtu nyimbo zote alizotoa ni nzuri, ni kali na twazipenda zote,” Diamond Platnumz alisema.

ameeleza sababu ya kuzozana na Alikiba
Diamond Platnumz ameeleza sababu ya kuzozana na Alikiba
Image: INSTAGRAM

Bosi wa WCB, Naseeb Abdul Juma almaarufu Diamond Platnumz ameweka wazi kuwa migogoro inayodaiwa kati yake na baadhi ya wasanii wenzake wa bongo fleva sio jambo zito.

Wakati akizungumza na Ayo TV, mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 32 alifichua kuwa matusi ya hadharani na wasanii wenzake kama vile Alikiba yana lengo la kusisimua tasnia ya muziki wa bongo.

Diamond alibainisha kuwa tasnia hiyo imelala kwa muda mrefu na hivyo wakati mwingine inahitajika kitu kitakacholeta uhai kwake na kuipa nguvu ya kuendelea.

“Najivunia kila mwanamuziki. Kwa kweli wanamuziki wengine tunazinguana lakini sio serious, kwangu it’s nothing serious. Tunacharuana, mchezo ulikuwa umelala sana, lazima tuamshe,” Diamond alisema.

Mwimbaji huyo alibainisha kuwa mikwaruzano yake ya hivi karibuni na mwenzake Alikiba yamepata matokeo chanya akitoa mfano wa shoo yake ya hivi majuzi ambayo ilivutia mashabiki wengi na kujaa msisimko.

Wakati huo huo, bosi huyo wa WCB alionekana kumkubali mpinzani wake mkuu, Alikiba na kubainisha kuwa nyimbo zake pia ni nzuri.

“Pongezi kwa kila mtu, kila mtu nyimbo zote alizotoa ni nzuri, ni kali na twazipenda zote,” Diamond Platnumz alisema.

Diamond bila shaka ni miongoni mwa wasanii watatu wakubwa zaidi kwenye tasnia ya muziki wa bongo fleva. Bosi wa King’s Music Alikiba na msanii wake wa zamani katika WCB, Rajab Abdul Kahali almaarufu Harmonize ambaye sasa anamiliki Konde Music Worldwide kwa muda mrefu wamechukuliwa kuwa wapinzani wake wakuu na katika siku za nyuma amehusika katika mizozo ya na wote wawili hao, huku hivi majuzi akishiriki vita vya mtandaoni na Alikiba.

Wikendi, mastaa hao wawili wa bongo walionekana kurudi kwenye mzozo wao ya muda mrefu.

Mwezi uliopita, Diamond aliweka wazi kwamba angetoa vibao baada ya vibao na kutangaza kwamba wasanii wengine wanapaswa kukaa mbali kwani hawataweza kumshinda.

Hili halikumpendeza Alikiba ambaye aliwataka mashabiki wake watazame na kuona.

Tweet ya Alikiba ya Jumapili ilionekana kutupa vijembe kwa Diamond Platnumz, ambaye alimtaja kuwa ni Quavo feki anayehitaji mafunzo ya sauti.

Diamond pia alimshambulia bosi huyo wa King’s Music kupitia ukurasa wake wa Instagram siku ya Jumapili na Jumatatu ambapo alimshushia heshima na kumtupia tuhuma nzito.