Ronaldo afikisha wafuasi milioni 600 kwenye Instagram, fahamu mamilioni anayopata kwa kila chapisho

Ronaldo ameweka historia ya kuwa wa kwanza kujizolea zaidi ya wafuasi milioni 600 kwenye Instagram.

Muhtasari

•Messi wa Argentina ndiye staa wa pili mwenye wafuasi wengi zaidi kwenye mtandao huo akiwa na wafuasi milioni 482.

• Ronaldo anapata angalau $3.23 milioni ambayo inatafsiri kuwa Sh463, 828, 000 kwa kila chapisho la Instagram.

Christiano Ronaldo
Image: HISANI

Mshambulizi wa Al Nassr Cristiano Ronaldo ameweka historia ya kuwa mtu wa kwanza kujizolea zaidi ya wafuasi milioni 600 kwenye Instagram.

Lionel Messi wa Argentina ndiye staa wa pili mwenye wafuasi wengi zaidi kwenye mtandao huo akiwa na wafuasi milioni 482, huku mwanamuziki Selena Gomez akiwa wa tatu na wafuasi milioni 427.

Mwanamitindo mashhuri Kylie Jenner (398M), Dwayne "The Rock" Johnson (388M), Ariana Grande (378M), Beyonce (315M), Khloe Kardashian (363M), Justin Bieber (293M) ni baadhi ya mastaa wengine walioingia kwenye 10 bora ya orodha ya watu wanaofuatiliwa zaidi kwenye mtandao wa Instagram.

Kulingana na Orodha ya Instagram Rich List ya 2023 iliyotengenezwa na Hopper HQ, Ronaldo anapata angalau $3.23 milioni ambayo inatafsiri kuwa Sh463, 828, 000 kwa kila chapisho la Instagram.

Mwezi Februari 2022, Ronaldo alikuwa mtu anayefuatiliwa zaidi kwenye mitandao ya kijamii ya kuchapisha picha na video, lakini idadi yake imeongezeka kwa kasi katika kipindi cha miezi.

Ronaldo pia alisherehekea siku yake ya kuzaliwa ya 37 Februari mwaka huu.

Katika Afrika Mashariki, Mkurugenzi Mtendaji wa Wasafi Media na mwimbaji Diamond Platnumz ndiye anayefuatwa zaidi akiwa na wafuasi milioni 16.

Katika kizazi hiki, nambari za Instagram ni kitu cha kujivunia, kwani watu wenye idadi kubwa hutumiwa kushawishi na kutangaza bidhaa na makampuni.

Watangazaji ambao wanataka bidhaa na huduma zao ziwafikie watu wengi iwezekanavyo watawasiliana na watu walio na ufuasi mkubwa kila wakati na hiyo inamaanisha pesa.