Shangwe Embu huku aliyekuwa rais Nigeria, Goodluck Jonathan akihudhuria harusi ya mpwa wake

Jonathan aliwashukuru watu wa Embu na kuahidi kwamba watamtunza binti yao vyema.

Muhtasari

•Jonathan alikaribishwa kwenye ukumbi wa harusi na wazee wa jamii ya Embu wakiongozwa na msemaji wao Njeru Kathangu.

•Jude  alipewa jukumu la kumtambua mkewe kutoka kwa kundi la wanawake sita ambao wote walikuwa wamefunikwa na leso.

alihudhuria harusi ya mpwa wake Jude Barristo siku ya Jumamosi
Goodluck Jonathan alihudhuria harusi ya mpwa wake Jude Barristo siku ya Jumamosi
Image: HISANI

Rais wa zamani wa Nigeria, Goodluck Jonathan alikuwa katika Kaunti ya Embu nchini Kenya siku ya Jumamosi ambapo alihudhuria harusi ya kitamaduni ya mpwa wake, Jude Barristo Ogbuku  katika Hoteli ya Izaak Walton.

Goodluck Jonathan ambaye aliondoka mamlakani mwaka wa 2015 baada ya kuhudumu kama rais wa Nigeria kwa takriban miaka mitano alikaribishwa kwenye ukumbi wa harusi na wazee wa jamii ya Embu wakiongozwa na msemaji wao Njeru Kathangu ambaye ni mbunge wa zamani wa Runyejes. Jonathan alikuwa amevalia suti nyeusi na kofia yake maarufu aina ya ‘godfather’.

Video na picha za harusi hiyo ya kusisimua zinamuonyesha rais huyo wa zamani na wageni wengine wakiongozwa na wazee wa Embu kuelekea kwenye mahema ambapo ilifanyika harusi hilo la kitamaduni.

Hafla hiyo ilipong’oa nanga, bwana harusi aliyetambulika kama Jude Barristo Ogbuku alipewa jukumu la kumtambua mke wake Joy Wanjiru Kamwithi kutoka kwa kundi la wanawake sita ambao wote walikuwa wamefunikwa na leso kuanzia kichwani hadi miguuni. Hakuchukua hata dakika tano kumtambua mpenzi huyo wake kisha wakaendelea kuketi pamoja.

Harusi hiyo ilijumuisha mchanganyiko wa tamaduni za Nigeria na Kenya. Wacheza ngoma za kitamaduni wa Embu waliwatumbuiza wageni kwa muziki wa kusisimua katika hafla hiyo.

Bibi harusi, Bi Joy Wanjiru ni binti ya aliyekuwa mbunge wa Runyenjes, marehemu Kamwithi Munyi. Mbunge wa zamani, Njeru Kathangu alimsimamia marehemu baba yake Wanjiru wakati wa hafla hiyo ya kitamaduni.

Katika hotuba yake mbele ya wageni, rais mstaafu Goodluck Jonathan ambaye pia alikuwa anamwakilisha babake bwana harusi aliwashukuru watu wa Embu na kuahidi kwamba watamtunza binti yao vyema.

Bw Jude na Wanjiru waliamua kufanya upya viapo vyao vya ndoa baada ya kuzuru Kenya kwa likizo. Wawili hao wamekuwa wakiishi pamoja na tayari wamejaliwa watoto wanne wa kiume ambao pia walikuwa kwenye harusi hiyo.