Hisia zatanda Gidi akieleza dhana ya kifo kwa binti yake mdogo (+video)

Marie-Rose alionekana mwenye hisia sana baada ya kusikia kuhusu hatima ya nyanya ya baba yake na akamfariji.

Muhtasari

•Gidi alisikika akijaribu kueleza dhana ya kifo kwa malkia huyo mdogo, jambo ambalo alikiri si rahisi kwake.

•Kwa maelezo hayo, malkia huyo mdogo alionekana kuelewa mfano ambao mtangazaji huyo mashuhuri alitumia kuelezea dhana ya kifo.

Gidi na binti yake Marie-Rose
Image: INSTAGRAM// GIDI OGIDI

Jumanne asubuhi, mtangazaji wa kipindi cha Gidi na Ghost Asubuhi asubuhi kwenye Redio Jambo, Gidi Ogidi alishiriki video ya matukio yenye hisia kali na bintiye Marie-Rose.

Katika video hiyo aliyoichapisha kwenye ukurasa wake wa Instagram, mtangazaji huyo mahiri alisikika akijaribu kueleza dhana ya kifo kwa malkia huyo mdogo, jambo ambalo alikiri si rahisi kwake.

"Sehemu ngumu zaidi ni kuelezea dhana ya kifo kwa mtoto," Gidi aliandika.

Mwimbaji huyo wa zamani alisikika kwenye video hiyo akitumia mfano wa marehemu nyanyake kumueleza binti yake kile kinachotokea baada ya kifo.

“Ukifa unazikwa. Nyanya yangu alikufa na akazikwa. Kwa hiyo, nyanya yangu hayupo tena,” Gidi alimwambia bintiye.

Kufuatia hilo, Marie-Rose ambaye alionekana mwenye hisia sana baada ya kusikia kuhusu hatima ya nyanya ya baba yake, alimfariji.

"Pole sana baba," alisema.

Gidi akajibu,”Asante mama, asante sana kwa kunipa pole. Lakini nyanya yako ni mama yangu, na nyanya yako yupo. Yuko hai. Kwa hiyo, ni nyanya yangu aliyefariki, lakini nyanya yako yupo.”

Kwa maelezo hayo, malkia huyo mdogo alionekana kuelewa mfano ambao mtangazaji huyo mashuhuri alitumia kuelezea dhana ya kifo.

Mwaka jana wakati msichana huyo akitimiza miaka sita, Gidi alitumia siku hii kumhakikishia  kuhusu upendo wake mkubwa kwake.

Alitaja siku ya kuadhimisha kuzaliwa kwa bintiye kama siku maalum sana  huku akimtakia hekima na maarifa zaidi anapoendelea kukua.

"Hii ndiyo siku ambayo Bwana ametengeneza. Marie-Rose anatimiza umri wa miaka 6 leo. Kheri za siku ya kuzaliwa nya Kanyamwa. Naomba ukue na maarifa na hekima ili kuleta mabadiliko katika dunia hii.Papa anakupenda," Gidi alimwandikia bintiye kupitia Instagram mnamo Mei mwaka jana.

Marie-Rose ni binti wa mtangazaji huyo mwenye uzoefu mkubwa ambaye anaishi na mama yake nchini Ufaransa.