“Nitalia!” Nadia Mukami afichua mambo anayoogopa mwanawe kumfanyia anapokua

Nadia amekiri kwamba ametiwa hofu sana na maendeleo ya haraka ya mwanawe wa pekee, Haseeb Kai.

Muhtasari

•Nadia alisema anahofia kwamba hivi karibuni anaweza kuanza kumtaka abishe mlango wake kabla ya kuingia au hata kumtaka akome kumbusu.

•Wakati huo huo, pia alidokeza kuhusu uhusiano wa karibu sana na wenye nguvu kati yake na Kai.

Nadia Mukami na mwanawe Haseeb Kai
Image: INSTAGRAM// NADIA MUKAMI

Malkia wa muziki wa Kenya Nadia Mukami amekiri kwamba ametiwa hofu sana na maendeleo ya haraka ya mwanawe wa pekee, Haseeb Kai.

Katika ukurasa wake wa Instagram, mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 26 alichapisha picha za Kai ambaye amekua sana na katika maelezo yake akabainisha kuwa mvulana huyo mwenye umri wa mwaka mmoja unusu anakua zaidi kila siku.

Wakati huo, Nadia alifichua kuwa kwa vile mwanawe anakua, anahofia kwamba hivi karibuni anaweza kuanza kumtaka abishe mlango wake kwanza kabla ya kuingia au hata kumtaka akome kumbusu wakati wowote akidai kuwa ni aibu.

"Ninaogopa kwamba anakua na hivi karibuni atasema mama tafadhali bisha au hata kusema mama achana na chum (busu) unaniaibisha," Nadia Mukami alisema.

Mama huyo wa mtoto mmoja alibainisha kwamba kusikia amri kama hizo kutoka kwa mwanawe kunaweza kumfanya azidiwe na hisia hadi kulia.

Wakati huo huo, pia alidokeza kuhusu uhusiano wa karibu sana na wenye nguvu kati yake na Kai.

“Nimezidiwa na upendo!! Ikiwa niliwahi kumhukumu Kijana wa mama tafadhali. Nisamehe! Sasa najua vizuri zaidi!!,” alisema.

Mwezi Machi mwaka jana, Nadia Mukami na mpenzi wake Arrow Bwoy walimkaribisha  mtoto wao Haseeb Kai duniani.

"24.03.2022 tumepokea zawadi nzuri zaidi Haseeb Kai. Karibu kwenye ulimwengu wetu," Arrow Bwoy alitangaza kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Hapo awali wanandoa hao walikuwa wamepoteza ujauzito wa ambaye angekuwa mtoto wao wa kwanza.

Kupitia Youtube Channel yake, Nadia alifichua kwamba alipoteza ujauzito wake wa kwanza mnamo Aprili 12, 2021.

Alifichua kuwa alikumbwa na huzuni kubwa kutokana na tukio hilo la kutisha  hadi kulazimika kupata ushauri wa kisaikolojia.

"Ulikuwa wakati mgumu kuwahi pitia. Huo ndio wakati nilitamani singekuwa msanii. Hospitalini nilioshwa, nilipotoka bado nilikuwa na trauma. Nilipitia kiwewe hadi nikaenda kupata ushauri. Nilikuwa naenda kupata ushauri na watu hawakujua, huo ndio wakati nilikuwa natengeneza ofisi yangu. Nilishauriwa sana na ilisaidia sana," Nadia alisimulia.

Katika kipindi hicho, mama huyo wa mtoto mmoja alijaribu sana kuficha hisia zake na kujifanya kama kwamba yupo sawa.

Msanii huyo hata hivyo alibahatika kupata ujauzito mwingine takriban miezi miwili baada ya kupoteza ule wa kwanza