Akothee afunguka kuhusu masaibu ya kushirikiana malezi na wapenzi wa zamani

Kwa sasa Akothee yuko Ufaransa ambako wanawe wawili wadogo wanaishi na mzazi mwenzake wa mwisho, Bw Dominic Decherf.

Muhtasari

•Akothee amebainisha kuwa kushirikiana katika jukumu la malezi kunahitaji uvumilivu, ustahimilivu na uelewano ili kufanikiwa.

•Jumatano, alishiriki siku na wanawe na akaenda nao kwenye hoteli ambapo walikula pamoja kabla ya kuelekea kwenye sinema kutazama filamu pamoja.

Akothee na wanawe Prince Oyoo na Prince Ojwang
Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Mwanamuziki na mjasiriamali wa Kenya Esther Akoth almaarufu Akothee amedokeza kwamba kushirikiana katika malezi na wapenzi wa zamani sio kazi rahisi.

Katika taarifa kwenye ukurasa wake wa Instagram siku ya Jumatano, mama huyo wa watoto watano ambaye kwa sasa yuko nchini Ufaransa kuwatembelea wanawe wawili wadogo, Prince Ojwang na Prince Oyoo alidokeza kuwa uzazi mwenza humnyenyekeza mtu na kumfundisha masomo kadhaa ya maisha.

Mwanamuziki huyo alibainisha kuwa kushirikiana katika jukumu la malezi kunahitaji uvumilivu, ustahimilivu na uelewano ili kufanikiwa.

“Mahusiano yatakupa ukuaji wa tabia, Ulezi mwenza utakunyenyekeza na kukufundisha uvumilivu, uelewano na ustahimilivu. Utalazimika kuvumilia wazimu unaokuja na malezi,” Akothee alisema.

Mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 43 alidokeza kwamba katika malezi ya kushirikiana, wazazi wote wawili wanapaswa kuvumiliana na kila mmoja bila kujali chochote kwa ajili ya ustawi wa watoto.

"Hapa kwa watoto hakunanga kwenye huyo mwingine🤣🤣🤣 mnakanyagana tu hapa hapa kwa ajili ya furaha ya watoto wenu, kuepuka na kupunguza drama," alisema.

Kwa sasa Akothee yuko nchini Ufaransa ambako watoto wake wawili wadogo wanaishi na mzazi mwenzake wa mwisho, Bw Dominic Decherf. Aliondoka nchini mapema wiki hii kuwatembelea wavulana hao wawili na kukaa nao baada ya kuwa mbali nao kwa muda.

Siku ya Jumatano, alishiriki siku nzima na wanawe na akaenda nao kwenye hoteli ambapo walikula chakula pamoja kabla ya kuelekea kwenye sinema kutazama filamu pamoja.

"Majukumu ya mama," aliandika chini ya video aliyochapisha Instagram ambayo ilimuonyesha akiwa na wavulana hao wawili katika mkahawa ambapo walikula kuku.

Mwishoni mwa mwezi uliopita, Akothee aliwashangaza wengi baada ya kufichua kuwa ana kikundi cha WhatsApp na wazazi wenzake.

Mama huyo wa watoto watano aliowapata na wanaume watatu tofauti alifichua hayo wakati akimsifia meneja wake na ambaye ni mpenzi wake wa zamani, Nelly Oaks mbele ya wageni wachache waalikwa waliokuwa wamehudhuria uzinduzi wa biashara ya bintiye Vesha Akello siku ya Jumamosi jioni.

Alikuwa akitambua majukumu makubwa ya Nelly Oaks na kueleza kwa nini si rahisi kuwa meneja wake.

"Niruhusu nimtambulishe mwanamume aliye nyuma ya chapa yangu, rafiki yangu bora. Jamaa huyu ana moyo mkubwa, kumshughulikia Akothee si kitu karibu na kumshughulikia Raila au Uhuru au Ruto,” Akothee alisema.

Aliongeza, "Kushughulikia mwanamke aliye na kikundi cha WhatsApp na baba wa watoto, mbwembwe, muziki.. tafadhali mpigieni makofi Nelly Oaks ."

Hata hivyo, hakufichua maelezo mengi kuhusu kikundi hicho cha WhatsApp na ikiwa kinajumuisha wazazi wenzake wote ama jinsi kinavyofanya kazi.