"Sio haki!" Mkewe Mr Seed, Nimo Gachuiri awakashifu walioshambulia familia ya Bahati

Nimo alibainisha kuwa Bahati na Diana huenda hawakuathiriwa na watu kuwashambulia wao kwani tayari wamepitia mengi.

Muhtasari

•Nimo alisema kuwa kitendo cha kuzifanyia ukarabati picha watoto wa wanandoa hao na kuwaweka pamoja na watu wengine mashuhuri si jambo jema.

•Wacha watu wastick kwa wazazi na wasiingize watoto. Mambo mengine wanayoandika hayana uhalisia na ni kukosa kazi. Hiyo si haki," alisema Nimo.

Diana Marua na Nimo Gachuiri
Diana Marua na Nimo Gachuiri
Image: HISANI

Nimo Gachuiri, mke wa mwanamuziki Mr Seed amelaani kitendo cha watu kuwashambulia Bahati, mke wake Diana Marua na watoto wao.

Wakati akizungumza na waandishi wa habari katika hafla, mama huyo wa mtoto mmoja alisema kuwa kitendo cha kuzifanyia ukarabati picha watoto wa wanandoa hao na kuwaweka pamoja na watu wengine mashuhuri si jambo jema.

Kutokana na hilo, Bi Nimo aliwataka watu wasiwahi kuwaingiza watoto kwenye mizozo yao na wazazi wao.

"Hiyo si nzuri, chochote ambacho wanafanya kwa sababu ninahisi kama wakati mtoto wangu alikuwa akishambuliwa, hilo ndilo jambo ambalo lilikuwa linaniumiza zaidi," Nimo alisema.

Aliongeza, “Wacha watu wastick kwa wazazi na wasiingize masuala na watoto. Mambo mengine wanayoandika hayana uhalisia na ni kukosa kazi. Hiyo si haki.

Mwimbaji huyo hata hivyo alibainisha kuwa Bahati na Diana huenda hawakuathiriwa na watu kuwashambulia wao kwani tayari wamepitia mengi.

"Nahisi kama kufikia sasa, familia ya Bahati wamepitia mengi kwa hivyo sidhani kuna chochote watahisi hata watu wakiphotoshop, sijui wafanye nini ati itawaingia kwenye ngozi sana," alisema Nimo.

Wiki iliyopita, mwimbaji Bahati aliihakikishia familia yake kuhusu upendo wake kwao kufuatia mashambulizi kwenye mitandao ya kijamii.

Katika barua kwa mwanawe wa kulea Morgan, Bahati alimhakikishia kijana huyo mwenye umri wa miaka 13 kwamba yeye ndiye baba yake licha ya mambo yote hasi yaliyosemwa kwenye mitandao ya kijamii.

Kuthibitisha kujitolea kwake na upendo wake kwake mwimbaji huyo alichukua fursa hiyo kusimulia safari ndefu ambayo wametembea pamoja tangu amchukue kutoka kwa nyumba ya watoto takriban miaka kumi iliyopita.

"Nimeitazama picha hii na nikagundua kuwa unakuwa Mwanaume. Hii ni miaka 10 iliyopita, siku ya kwanza nilipokutana nawe. Siku hiyo nilipoalika ABC Children's Home (ambapo nilikulia) kuja na kutumbuiza katika Uzinduzi wa Albamu yangu mwaka wa 2013 katika NPC Valley Road. Mwana nakumbuka siku ile kama Jana; jinsi ulivyolia na kuniita baba. Ilikuwa ngumu sana kwangu kuona wewe ukiwa na miaka 2 ukilazimisha kuingia kwenye basi linalorudi kwenye kituo cha watoto yatima; Niliona uchungu wako na nikajiona kupitia kwako; Kwa kuwa nimekua katika Nyumba ya Watoto wakati fulani, nikiwa pweke bila mtu wa Kumwita Mama au Baba!,” Bahati alisimulia chini ya picha zilizoonyesha ukuaji wa Morgan tangu walipokutana kwa mara ya kwanza hadi sasa.

Akaendelea, ” Mwanangu tangu siku ile; ingawa sikuwa tayari niliamua kuwa baba na nikakuchukua kama mwanangu. Mwana Nisikilize! Mimi ni Baba yako na Wewe ni Mwanangu! Mungu Alipanga Hakuna Kitu Kinachoweza Kubadili Hilo! Unapokua utaona mambo mengi ya Upuuzi na ya kinyama yanayosemwa kwenye Ulimwengu huu usio na huruma lakini kila wakati kumbuka licha ya yote, MIMI NI BABA YAKO NA WEWE NI MWANANGU! Mungu pekee ndiye Ajuaye yale tuliyopitia.”