Bobi Wine amsherehekea mke wake Barbie kwa ujumbe mtamu

Mwanasiasa huyo amemshukuru mkewe kwa kumjenga na kwa mchango wake mkubwa katika maisha yake.

Muhtasari

•"Kila mara nirudipo nyumbani nikiwa nimedhoofika, unanidekeza na kunitayarisha kwa pambano la siku inayofuata," Wine alisema.

•Barbie alichangia pakubwa sana katika umaarufu wa Bobi kisiasa, kwa kumpigia upato kwenye sakasaka zake za kura 2018 na 2020 

Bobi Wine na Mke wake Barbie
Bobi Wine na Mke wake Barbie
Image: Facebook/Bobi Wine

Mwana siasa maarufu wa nchi ya Uganda,Robert Kyagulanyi Ssentamu anayekwenda kwa jina la Bobi Wine, amemuandikia mkewe Barbie Kyagulanyi, ujumbe wa kheri ya siku ya kuzaliwa wenye hisia nzito.

Bobi Wine kwenye ujumbe  aliochapishwa kwenye ukurasa wake wa Instagram alisema;

"Ulimjenga Mume wako kwa ukamilifu, kisha ukamuachilia kwa taifa bila kusitasita, kila mara nirudipo nyumbani nikiwa nimedhoofika, unanidekeza na kunitayarisha kwa pambano la siku inayofuata.

Leo ni siku yako ya kuzaliwa, nasikitika badala ya kukupeleka kwenye kikao cha chakula cha jioni cha mahaba,ila niko mbali na Lira kwa shughuli za kuwanufaisha wote, lakini najua hilo halitakukera.

Mpendwa Barbie Kyagulanyi, kwa niaba ya Taifa lenye shukrani,ASANTE.

Heri ya siku ya kuzaliwa kwako, Mpenzi wa maisha yangu,"

Barbie Kyagulanyi,ni mwanaharakati ambaye pia ni mwanzilishi wa mpango wa "Caring Hearts Uganda", ambao unaangazia uwezeshaji wa watoto katika uongozi, UKIMWI, usafi wa mazingira wakati wa hedhi ikiwa ni pamoja na elimu.

Kitabu chake cha Kumbukumbu za Dhahabu za Belle ya Kijiji 2012 kilimfanya kutambulika zaidi.

Barbie alikutana na Bobi Wine alipokuwa katika shule ya upili wakati ambapo Bobi alikuwa mwanafunzi wa muziki wa densi na maigizo katika Chuo Kikuu cha Makerere .

Wapenzi hawa wamekuwa kwa ndoa zaidi ya miaka kumi tangu waliopouasi ukapera mwaka wa 2011 kwenye kanisa la Rubaga Kampala.

Bobi na Barbie wamebarikiwa na watoto wanne.

Bobi Wine, ni mwanasiasa, mwimbaji, na mwigizaji wa Uganda. Aliwahi kuwa mbunge wa eneo bunge la kaunti ya kyadondo Mashariki iliyoko wilaya ya Wakiso,katika mkoa wa kati nchini Uganda.

Barbie alichangia pakubwa sana katika umaarufu wa Bobi kisiasa, kwa kumpigia upato kwenye sakasaka zake za kura 2018 na 2020 kwa manifesto yake kuhusu,akina mama, watoto na vijana.

Alipigania sana kuachiliwa kwa Bobi alipotiwa mbaroni wakati wa kampeni zake za urais za mwaka wa 2020.

Kwenye mahojiano na shirika la BBC, Barbie alisema; "Mapambano ya mabadiliko hayakuhusu yeye wala familia yake bali watu wanaokandamizwa nchini Uganda,"

Bobi,aligombea Urais nchini Uganda mwaka wa 2021 chini ya chama cha National Unity Platform ambacho anakiongoza.