Kutana na mmiliki wa nyumba ya Zimmerman inayovuma mitandaoni

Bi Lumbasi alibainisha kuwa nyumba hiyo ilichukua takriban miaka minne kujengwa na ilimgharimu mamilioni ya pesa.

Muhtasari

•Bi Lumbasi alibainisha kuwa kujenga nyumba yake ya kuishi juu ya nyumba za kukodisha lilikuwa wazo lake na liliungwa mkono na mjenzi wake.

•Alisema kuwa wazo la kujenga nyumba za kukodisha na nyumba ya kuishi lilichochewa na hamu yake ya kutumia kipande chake cha ardi kikamilifu.

katika mahojiano.
Bi Anne Lumbasi katika mahojiano.
Image: HISANI// PAXTON TV

Nyumba ya Bi Annie Lumbasi imekuwa ikivuma kwenye mitandao ya kijamii katika takriban wiki moja iliyopita kutokana na mtindo wake wa kipekee.

Uamuzi wa mjasiriamali na muuguzi  huyo wa Kenya ambaye anaishi Marekani wa kujenga jumba lake la kifahari juu ya nyumba za kupangisha amewashangaza wengi kwani sio jambo la kawaida sana.

Akiongea katika mahojiano na Paxson TV, mama huyo wa watoto watatu alibainisha kuwa kujenga nyumba yake ya kuishi juu ya nyumba za kukodisha lilikuwa wazo lake na liliungwa mkono na mjenzi wake.

"Nilileta wazo kwa mjenzi wangu. Aliniambia inawezekana, inaweza kufanyika. Aliniambia kuhusu bei, muda gani itachukua na vifaa vinavyohitajika. Tulifanya kazi pamoja, mkono kwa mkono. Alikuwa akiniuliza, ‘unataka tufanyeje hapa au pale?’ Nilikuwa namtumia barua pepe, nampigia simu nikimwambia tufanye hivi au vile,” Bi Lumbasi alisema.

Image: HISANI

Nyumba hiyo ambayo iko katika mtaa wa Zimmerman, Kasarani ilijengwa akiwa bado nchini Marekani na mawasiliano mengi na mjenzi wake yalikuwa kupitia simu.

Bi Lumbasi alisema amemfahamu mjenzi aliyemjengea nyumba yake kwa miaka mingi kwani  alikuwa akimjengea baba yake nyumba katika siku za nyuma.

"Nyumba imechukua miaka minne kujengwa. Ni kazi nyingi. Watu wanaona tu nyumba lakini ni kazi ngumu sana. Unapaswa kufanya kazi kwa bidii lakini zaidi ya yote unapaswa kuwa na imani na kumwamini Mungu,” alisema.

Pia alibainisha kuwa imemgharimu mamilioni ya pesa kujenga.

Mjasiriamali huyo alisema kuwa wazo la kujenga nyumba za kukodisha na nyumba ya kuishi lilichochewa na hamu yake ya kutumia kipande chake cha ardi kikamilifu.

Alisema kwamba aliamua kununua ardhi na kujenga katika mtaa wa Zimmerman kwani alikulia katika eneo hilo na alitaka kufufua maisha yake ya utotoni.

Licha ya wengi kusifu ubunifu wa mwenye nyumba hiyo wa kujenga nyumba za kukodisha chini ya nyumba yake ya kuishi, hakujakosa wakosoaji ambao wamedokeza baadhi ya mianya kwenye jengo hilo.

Bi Lumbasi hata hivyo amedokeza kuwa nyumba hiyo ni salama sana kwani utafiti na ushauri mwingi ulifanyika kabla ya ujenzi.