Sijavunja sheria yoyote, ndoa ya wake wengi ni halali!- Karen Nyamu atetea mahusiano na Samidoh

Karen Nyamu amekuwa akichumbiana na Samidoh licha ya mwimbaji huyo kuwa kwa ndoa na Edday Nderitu kwa zaidi ya muongo mmoja.

Muhtasari

•Akizungumza siku ya Jumatatu, Nyamu alisema anaamini hajavunja sheria yoyote kwa kuwa katika uhusiano wake.

•Bunge lilipitisha mswada unaoruhusu wanaume kuoa wake wengi mwezi Machi 2014.

Samidoh na Karen Nyamu
Image: FACEBOOK// KAREN NYAMU

Seneta wa kuteuliwa Karen Nyamu ametetea uhusiano wake na mwimbaji wa Mugithi Samuel Muchoki almaarufu Samidoh akisema sheria za Kenya zinaruhusu ndoa za wake wengi.

Akizungumza siku ya Jumatatu kwenye NTV, Nyamu alisema anaamini hajavunja sheria yoyote kwa kuwa katika uhusiano wake.

"Kuna sheria ya polygamy ambayo imepitishwa kwa Bunge yetu, sijavunja sheria yoyote kukuwa katika situation mimi niko," alisema.

Bunge lilipitisha mswada unaoruhusu wanaume kuoa wake wengi mwezi Machi 2014.

Muswada huo uliopitishwa Machi 20, 2014, ulirekebisha sheria ya ndoa na kurasimisha sheria ya kimila kuhusu kuoa zaidi ya mtu mmoja.

Mswada uliopendekezwa hapo awali ulikuwa umempa mke wa kwanza haki ya kuidhinisha chaguo la mumewe kwa mke wa pili, lakini wabunge wanaume waliungana na kupitisha marekebisho ambayo yalifuta kifungu hicho.

"Unapooa mwanamke wa Kiafrika, lazima ajue kuwa wa pili yuko njiani, na mke wa tatu ... hii ni Afrika," Mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohammed alisema wakati wa mjadala.

Ndoa za wake wengi hutokea sana nchini Kenya kama ilivyo katika nchi nyingi za Kiafrika na jamii nyingi za kitamaduni.

Inakubalika pia miongoni mwa jamii ya Kiislamu, ambao Sharia yao inaruhusu mwanamume kuoa hadi wake wanne lakini kwa ridhaa ya mke wa kwanza.

Nyamu aliwataka vijana kuwa vile wanavyotaka kuwa kwa kufanya wanachojua ni sahihi badala ya kushabikia watu.

Seneta huyo amekuwa na uhusiano na Samidoh licha ya mwanamuziki huyo tayari kuwa kwenye ndoa  na Edday Nderitu.

Hata hivyo, mwezi Julai Edday alisema kuwa hakuwa kwenye ndoa ya wake wengi na kutangaza kwamba alimuacha Samidoh na kuhamia Marekani na watoto wake anakoishi kwa sasa.

Edday alifafanua kwenye ukurasa wake wa Facebook kuwa hayupo tena kwenye ndoa na mwanamuziki huyo. Alisema uamuzi wake wa kuondoka Kenya ulikuwa kuwaokoa watoto wake kutokana na mazingira ya sumu.

"Nimeweza kushughulikia mahitaji ya watoto wangu hadi sasa bila usaidizi wowote na sijutii hata kidogo. Sihitaji drama yoyote, nahitaji amani," Edday alishiriki.

Alikiri zaidi kuwa alitaka ndoa ya faraghani lakini mwimbaji huyo aligeuza uhusiano kuwa wa hadharani kwa kujitokeza hadharani na Nyamu.

Edday alisema hii ilisababisha mambo kuwa makubwa sana.