Akothee ajawa na bashasha huku akipata digrii yake baada ya miaka 14 ya masomo

Akothee amejipongeza kwa kufaulu kumaliza kozi yake ya digrii baada ya miaka kumi na minne ya masomo.

Muhtasari

•Mwanamuziki huyo alisherehekea mafanikio hayo makubwa na kuyataja kama dhihirisho la ukakamavu usioyumbayumba.

•Akothee alianza masomo zaidi ya mwongo mmoja uliopita na ni miongoni mwa maelfu ya wahitimu watakaopokea taji lao mwaka huu.

Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Mwanamuziki na mfanyibiashara mashuhuri wa Kenya Esther Akoth almaarufu Akothee amejipongeza kwa kufaulu kumaliza kozi yake ya digrii baada ya miaka kumi na minne ya masomo.

Katika taarifa yake Ijumaa asubuhi, mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 43 ambaye anatazamiwa kuhitimu rasmi na Shahada ya Kwanza ya Usimamizi wa Biashara kutoka Chuo Kikuu cha Mt Kenya hivi leo, Desemba 8 alisherehekea mafanikio hayo makubwa na kuyataja kama dhihirisho la ukakamavu usioyumbayumba.

Akothee alianza kozi yake ya shahada katika chuo kikuu hicho cha kibinafsi zaidi ya mwongo mmoja uliopita na ni miongoni mwa maelfu ya wahitimu ambao watapokea taji lao mwaka huu.

“Leo, tunashuhudia ushindi wa miaka 14 tangu... Kuhitimu kwa ESTHER AKOTH KOKEYO kutoka chuo kikuu cha MT KENYA darasa la BBM la 2023 sio tu mafanikio ya kitaaluma; ni dhihirisho la ustahimilivu usioyumba,” Akothee alisema kupitia Instagram.

Aliongeza, “Katika kukabiliana na dhiki, safari ya Akothee inaashiria roho ya mwanadamu isiyoweza kushindwa. Kuhitimu kwake sio tu ushindi wa kibinafsi lakini msukumo kwa wote wanaothubutu kuota dhidi ya uwezekano wowote.

Hongera, ESTHER AKOTH KOKEYO AKOTHEE, kwa mafanikio haya ya ajabu💪 Uthabiti wako ni mwanga, unaoangazia njia kwa wale wanaoamini katika nguvu ya mabadiliko ya elimu. Hongera kwa safari iliyosafirishwa vyema na siku zijazo zilizojaa uwezekano usio na kikomo. Hongera sana MIN OYOO.”

Kufuatia kuhitimu kwake, mama huyo wa watoto watano amepanga kufanya karamu kubwa siku ya Jumamosi, Desemba 10 nyumbani kwake Rongo, kaunti ya Migori.

Katika mahojiano ya mapema mwaka huu, mwimbaji huyo alifichua kuwa mama yake ndiye sababu kuu iliyomfanya aamue kurejea chuo kikuu na kufanya digrii yake.

Akizungumza katika TV47 mapema mwezi uliopita, Akothee alisema ingawa alichuma pesa nyingi, maishani mamake hakumwacha apumzike.

"Hivi majuzi nilimaliza elimu yangu ya muda mrefu kutoka Chuo Kikuu cha Mount Kenya na kwa sasa nina shahada. Mama yangu ni mtu wa nidhamu na kila nilipomweleza mafanikio yangu; majumba ninayojenga, hundi zangu benki alibaki nazo. kuniuliza kuhusu shahada yangu," alisema.

Mwanamuziki huyo alisema amekuwa katika chuo kikuu kwa miaka 14 iliyopita na msukumo huo ulitoka kwa mama yake.

"Nadhani nilizaliwa msichana mwenye akilI na ninaamini kuwa sihitaji kusoma vitabU kuandika chochote kwenye karatasi yoyote. Hata hivyo nilihisi kama mama yangu alikuwa shingoni mwangu na ilikuwa bora kupata digrii ili awezE kupumzika," Akothee alisema.