Eric Omondi awaomba Wakenya wamsaidie Mwana Mtule kuachiliwa huru kutoka KNH

Mwana Mtule hawezi kuruhusiwa kwenda nyumbani kwa sababu ya bili ya karibu shilingi nusu milioni.

Muhtasari

•"Aliruhusiwa kutoka hospitalini kama mwezi mmoja uliopita lakini anazuiliwa hapa kwa sababu ya bili isiyolipwa ya Ksh450k," Eric Omondi alisema.

•Mwana Mtule alionekana akitembea kwa matatizo lakini akabainisha kuwa anajisikia vizuri zaidi na yuko tayari kurudi nyumbani.

Image: HISANI

Mchekeshaji Eric Omondi amewasihi Wakenya kumsaidia msanii mwenzake Peter Wangundi almaarufu Alpha Mwana Mtule kutoka katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta anakodaiwa kuzuiliwa kutokana na bili kubwa ambayo haijalipwa.

Katika taarifa yake siku ya Jumatatu, mchekeshaji huyo ambaye pia anajihusisha pakubwa na uanaharakati alifichua kuwa licha ya kuruhusiwa kutoka hospitalini takriban mwezi mmoja uliopita, Mwana Mtule hawezi kuruhusiwa kwenda nyumbani kwa sababu ya bili ya karibu shilingi nusu milioni.

“Huyu jamaa amepitia mengi kweli. TEAM SISI KWA SISI naomba tutoe hapa leo,” Eric Omondi alisema kupitia akaunti yake ya Instagram.

Aliongeza, "Aliruhusiwa kutoka hospitalini kama mwezi mmoja uliopita lakini anazuiliwa hapa kwa sababu ya bili isiyolipwa ya Ksh450k, hii tunaweza kuongeza saa hizi niende nimtoe aende nyumbani asikule Krismasi hapa. Namba yake ni 0725468373 (JINA: PETER WANGUDI). Tuma chochote unachoweza.”

Eric aliambatanisha taarifa yake na video yake akiwa na mwimbaji huyo wa nyimbo za injili ambaye amekuwa mgonjwa kwa miezi michache iliyopita.

Katika video hiyo, Mwana Mtule alionekana akitembea kwa matatizo lakini akabainisha kuwa anajisikia vizuri zaidi na yuko tayari kurudi nyumbani.

“Huyu ni Mwana Mtule na yuko tayari kutoka hospitalini, amepona. Yuko sawa. Amewekwa hapa juu ya 450,000. Leo tunamtoa,” Eric alisema kwenye video hiyo kabla ya kumtaka mwimbaji huyo kusema nambari yake ya simu.

Mchekeshaji Eric Omondi alizuru hospitali ya KNH baada ya Mwana Mtule kutoa wito kwa Wakenya kumsaidia kulipa bili ya hospitali iliyokuwa imesalia.

Katika taarifa yake mwimbaji huyo wa nyimbo za injili alisema, "Habari za familia, bado Bado nimefungiwa huku Kenyatta hospitali kwa sababu kutaka salio lao la 450k, nimeruhusiwa kutoka hospitali, Asanteni FAM mumenisaidia tukawalipa 462k ya matibabu.

Naomba munisaidie tumalizie hii balance yao ya 450k. Chochote ulicho nacho tafadhali nitumie tumalizie. Nambari yangu ya Mpesa ndo hii 07 25 46 83 73, jina ni PETER Wangudi. Kwa sasa tuko 17k. Tafadhali familia nisaidie nitoke huku Nimekua kama mfungwa wao tena 🙏."