Hisia huku mtangazaji Dr. King'ori akiondoka NTV, atangaza hatua yake inayofuata

Mtangazaji huyo mcheshi alitangaza kwamba Toleo la Ijumaa la The Wicked Edition lilikuwa la mwisho.

Muhtasari

•Mtangazaji Dr King’ori ameiaga NTV baada ya miaka saba ya kuandaa kipindi cha The Wicked Edition katika kituo hicho.

•King'ori alitangaza hatua yake inayofuata baada ya kuondoka NTV akidokeza bado atakuwa kwenye tasnia ya sanaa.

Image: INSTAGRAM// DR KING'ORI

Mtangazaji maarufu wa runinga Felix Omondi almaarufu Dr King’ori ameiaga NTV baada ya miaka saba ya kuandaa kipindi cha The Wicked Edition katika kituo hicho.

Katika taarifa yake ya siku ya Ijumaa jioni, mtangazaji huyo mcheshi alitangaza kwamba Toleo la wiki hii la The Wicked Edition lilikuwa la mwisho.

King’ori alisherehekea mafanikio yake mengi katika NTV na kuwashukuru mashabiki kwa sapoti kubwa ambayo walimpa kwa miaka mingi.

"Imekuwa miaka 7 ya mabadiliko na zaidi ya vipindi 300 visivyoweza kusahaulika kwenye TV na zaidi ya views milioni 70 kwenye YouTube na kufanya Wicked Edition kuwa kipindi cha kejeli cha muda mrefu zaidi kwenye televisheni ya Kenya," taarifa ya King'ori ilisema.

Aliongeza, “Tangu kuanzishwa kwake,  The Wicked Edition imekua ikionyesha ubora wa hali ya juu nchini Kenya. Ufadhili wako ulitufanya tufikie viwango vya juu zaidi na kutuletea kutambuliwa katika Tuzo za kifahari za Kalasaha na kuteuliwa kama vicheshi vya televisheni vinavyofanya vizuri zaidi na vicheshi bora zaidi vya televisheni nchini Kenya kwa toleo lijalo la 2024.”

Mchekeshaji huyo aliendelea kuishukuru NTV kwa nafasi hiyo na pia aliipongeza timu aliyofanya nayo kazi kwa usaidizi waliompa.

Pia alitangaza hatua yake inayofuata baada ya kuondoka kituo hicho kinachomilikiwa na Nation Media Group akidokeza kuwa bado atakuwa kwenye tasnia ya sanaa.

"Safari hii, huku tukimalizia na NTV Kenya, ni mwanzo mpya tunapopanua wigo wetu, kujitosa katika juhudi kubwa za ubunifu na kuendelea kuwasilisha maudhui yenye thamani kwa mashabiki wetu kote Afrika Mashariki na kwingineko," alisema.

Aliongeza, “Asanteni kwa kuwa sehemu ya hadithi yetu. Hapa ni kufungua ukurasa mpya pamoja na kutarajia hadithi nyingi ambazo bado hazijasimuliwa."

Mamia ya wanamtandao walijibu taarifa ya mchekeshaji huyo huku wengi wakimpongeza kwa hatua hiyo kubwa na wengine wakimtakia mafanikio mema.

Tazama maoni ya baadhi ya mashabiki;

Justina Wamae: This is growth. Congratulations on your new endeavor.

ML Rodger: Personally I enjoyed your shows bro, be blessed and to greater heights.

Maggie Gathoni: The only show I make time to watch.

Josphat Livondo: Kazi nzuri Dr. Kingori we wish you all the best on your future endeavors.

Ian Sitienei: One of the best show ever, we will really miss the show.