Chanzo cha kifo cha msanii maarufu wa Nigeria 'Mr. Ibu'

Rais wa Chama cha Waigizaji wa Filamu wa Nigeria, Emeka Rollas alithibitisha taarifa za kifo cha Bw. Ibu siku ya Jumamosi.

Muhtasari

• Mnamo Oktoba 2023, video ilisambaa kwenye mitandao ya kijamii ambapo kuna mvulana alionekana akiwauliza wapendwa wake wamjumuishe katika maombi.

Marehemu Mr. Ibu.
Marehemu Mr. Ibu.
Image: REALMRIBU/INSTAGRAM

Mchekeshaji maarufu wa Nigeria, John Okafor almaarufu Mr. Ibu amefariki dunia siku ya Jumamosi baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Bw. Ibu alifariki akiwa katika hospitali moja mjini Lagos alipokuwa akipatiwa matibabu.

Rais wa Chama cha Waigizaji wa Filamu wa Nigeria, Emeka Rollas alithibitisha taarifa za kifo cha Bw. Ibu siku ya Jumamosi.

Alieleza kwenye ukurasa wake wa Instagram kuwa:

“Ni kwa masikitiko makubwa nawatangazia kuwa bwana Ibu amefariki dunia. baada ya kusumbuliwa na tatizo la moyo kwa miaka 24.

Jinsi bwana Ibu alivyohangaika na matibabu

Mnamo Oktoba 2023, video ilisambaa kwenye mitandao ya kijamii ambapo kuna mvulana alionekana akiwauliza wapendwa wake wamjumuishe katika maombi.

Katika video hiyo, Bw. Ibu alisema kuwa amekaa kwa muda mrefu hospitalini kwa sababu ya ugonjwa "usiotibika.

Katika video hiyo, alisema kuwa madaktari walipendekeza kukatwa miguu yake.

Aliongeza kuwa “Kwa sasa bado naendelea na matibabu hospitalini, Mkuu wa hospitali hiyo alisema bora nikatwe mguu ikiwa wanachokwenda kukifanya hakitafanikiwa.

Kisha akawaomba wapendwa wake wamwombee ili asikatwe mguu wake.

Historia ya Bwana Ibu John Okafor

Mr.Ibu ni muigizaji na mchekeshaji ambaye alitokea Dabe katika jimbo la Enugu kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Ameonekana katika mamia ya sinema za Nollywood ndani na nje ya Nigeria.

Alipata umaarufu kwa jinsi alivyoweza kudhibiti uso wake anapotaka kuwachekesha watazamaji.

Kwa nyakati tofauti, alikuwa akicheza muziki na kucheka ili kuburudisha hadhira.

Mnamo Disemba 2023, familia ya Bw. Ibu ilieleza ugonjwa wake wakati ambapo habari zilisambaa mtandaoni kuwa miguu yote miwili ya bwana Ibu imekatwa.

Hata hivyo, mmoja wa wanafamilia yake aitwaye Valentine Okafor alisema kwenye ukurasa wake wa Instagram kwamba mguu wa Bw. Ibu ulikatwa.

Familia hiyo pia ilieleza ukweli kuhusu ugonjwa wake, ikisema kuwa yeye haugui kisukari, lakini “mara nyingi anatokwa na damu miguuni (kuharibika kwa mishipa ya damu)” na magonjwa mengine yanayotishia maisha yake.