Tutawatafutia kazi: Erick Omondi aahidi vijana wasio na kazi

Takriban ujumbe zote zilikuwa na kitu sawa zikimsihi mchekeshaji awasaidie kupata kazi.

Muhtasari
  • Mchekeshaji huyo amezindua mpango uliopewa jina la Chama cha Ajira cha Kenya katika jitihada za kupunguza kiwango cha ukosefu wa ajira nchini.
Eric Omondi
Eric Omondi
Image: Facebook

Mwanaharakati Erick Omondi ameonyesha zaidi ya jumbe 12,000 ambazo hazijasomwa alizopokea kutoka kwa vijana wa Kenya wasio na ajira.

Kupitia mtandao wa instagram, mfadhili huyo alipitia jumbe zilizotumwa na nambari ambazo hazijahifadhiwa kwa nasibu kwenye nambari yake ya whatsapp.

Takriban ujumbe zote zilikuwa na kitu sawa zikimsihi mchekeshaji awasaidie kupata kazi.

Nimepokea jumbe 12,400 kutoka kwa Wakenya wasio na ajira leo na bado nahesabu!! Niamini. Tutawatafutia watu hawa ajira. Tutawaunganisha waajiri wa Kenya na wasio na ajira. Tutawasaidia ndugu na dada zetu kupata riziki zao, aliandika.

Mchekeshaji huyo amezindua mpango uliopewa jina la Chama cha Ajira cha Kenya katika jitihada za kupunguza kiwango cha ukosefu wa ajira nchini.

Akizungumza katika video iliyoshirikiwa kwenye ukurasa wake wa instagram, mcheshi huyo alisema karibu nusu ya watu wa Kenya hawana kazi hivyo kufanya iwe vigumu kwa familia nyingi kujikimu na kuishi maisha ya starehe.

"Karibu nusu ya wakazi wa Kenya hawana ajira. Wanaume wengi hawawezi kuhudumia wake zao. Kuweka chakula mezani limekuwa suala katika nchi hii na ni kwa sababu ya kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira",  Erick alisema.

Akitoa wito kwa waajiri, Erick aliomba kwamba yeyote aliye na fursa bila kujali aina ya kazi anafaa kuwa tayari kuajiri Wakenya ili kusaidia katika hali ya ukosefu wa ajira nchini.

"Ikiwa wewe ni mwajiri, ukiwa na kazi yoyote, inaweza kuwa ya kazi ya nyumbani, fundi, nesi, daktari, mwanasheria hata mtu wa mjengo. Ikiwa una mahali fulani unapojenga na unahitaji mfanyakazi wa kawaida wa kubeba vitalu au mbao, tafadhali toa maoni yako hapa chini. Tutaanzisha vuguvugu, aina ya chama ambacho tunakipa jina, chama cha Ajira cha Kenya. Jukwaa hili tunalolianzisha leo linakwenda kuleta mapinduzi ya ajira nchini", alisema.