"Heshima kubwa zaidi ya maisha yangu!" Jacque Maribe ajivunia ukuaji wa mwanawe

Maribe alimsherehekea mwanawe Zahari Maribe alipoadhimisha miaka kumi yake ya kuzaliwa.

Muhtasari

•Maribe ambaye hivi majuzi aliondolewa mashtaka ya mauaji alimtaja mwanawe kama heshima kuu maishani mwake.

•Pia alionyesha fahari yake kubwa katika ukuaji wa mvulana huyo.

Jacque Maribe na mwanawe
Image: Hisani

Mtangazaji wa habari za TV wa zamani Jacque Maribe alimsherehekea mwanawe Zahari Maribe alipoadhimisha miaka kumi yake ya kuzaliwa.

Katika taarifa fupi siku ya Jumanne, mwanahabari huyo maarufu ambaye hivi majuzi aliondolewa mashtaka ya mauaji alimtaja mwanawe kama heshima kuu maishani mwake.

Pia alionyesha fahari yake kubwa katika ukuaji wa mvulana huyo.

"Zahari, heshima kubwa zaidi ya maisha yangu. Kheri ya siku ya 10 ya kuzaliwa.. tumefanikiwa @ZAHARIMARIBE,” Bi Maribe alimwandikia  mwanawe kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Zahari ndiye mtoto pekee wa mtangazaji habari huyo wa zamani wa runinga ya Citizen.

Maribe aliondolewa mashtaka katika kesi ya mauaji ya Monica Kimani mnamo Februari 9, 2024, na Jaji Grace Nzioka wa Mahakama ya Milimani kwa kukosa ushahidi.

Kulingana na Jaji Nzioka, shtaka lililowasilishwa dhidi ya Maribe halikuwekwa ipasavyo.

"Ni maoni yangu kwamba shtaka lililoletwa dhidi ya mshtakiwa wa pili halikuwa shitaka sahihi," alisema.

Maribe alikuwa ni mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo ambayo ilikuwa ikiendelea kwa zaidi ya miaka mitano.

"Je, kulikuwa na kosa lolote wakati mshtakiwa wa pili alipoeleza afisa wa uchunguzi katika kituo cha polisi cha Lang'ata jambo ambalo si kweli? Sisemi zaidi. Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma inajua wajibu wao. “

Matokeo yake ni kwamba upande wa mashtaka haukutoa ushahidi wa kutosha kwa mahakama hii kumpata mshtakiwa wa pili na hatia ya kosa la mauaji ya Monica Nyawira Kimani usiku wa Septemba 19, 2018,” Hakimu Nzioka alisema.

Jaji Nzioka, hata hivyo, alisema upande wa mashtaka ulitoa ushahidi wa kutosha dhidi ya mshtakiwa wa kwanza, Jowie Irungu na ulitimiza kizingiti.

"Mtu aliyemuua marehemu hakukusudia kumpa hata dakika moja ili aokoke. Ni maoni yangu na kugundua kuwa mhusika alikusudia kifo cha papo hapo," alisema.

"Ushahidi huu wote uliochukuliwa unaacha hitimisho kali kwamba Irungu alimuua Monica Kimani."