Gidi atoa ushauri maalum kwa Butita baada ya kuandamana na rais Ruto, kukutana na mastaa wakubwa

Gidi amesema Butita kukutana na rais Ruto na mastaa wa kimataifa nchini Marekani si hakikisho la mafanikio.

Muhtasari

•Katika taarifa yake ya Alhamisi, Gidi alibainisha kuwa Butita anapaswa kutumia fursa hizo vizuri ili kuvuna mafanikio.

•Butita anafurahia wakati nchini Marekani ambapo ameandamana na Rais William Ruto katika safari yake ya kikazi.

ametoa ushauri maalum kwa mchekeshaji Eddie Butita.
Gidi ametoa ushauri maalum kwa mchekeshaji Eddie Butita.
Image: HISANI

Mtangazaji mahiri wa kipindi cha Gidi na Ghost asubuhi kwenye Radio Jambo Gidi Ogidi amebainisha kuwa mchekeshaji Eddie Butita kukutana na rais William Ruto na watu mashuhuri wa kimataifa nchini Marekani si hakikisho la mafanikio.

Katika taarifa yake ya Alhamisi asubuhi, mwimbaji huyo wa zamani alibainisha kuwa Butita anapaswa kutumia fursa hizo vizuri ili kuvuna mafanikio.

“Lakini kwa nini tunahitimisha kuwa Butita amefanikiwa? Kukutana na Rais na watu mashuhuri wa Marekani sio hakikisho la mafanikio, ni kile atakachofanya kutokana na fursa hizo ndicho kitamfanya afanikiwe,” Gidi alisema kupitia ukurasa wake wa Facebook.

Haya yanajiri wakati mchekeshaji Eddie Butita akifurahia wakati nchini Marekani ambapo ameandamana na Rais William Ruto katika safari yake ya kikazi.

Mchekeshaji huyo wa zamani wa Churchill Show ni miongoni mwa wajumbe wanaoandamana na Rais William Ruto katika safari hiyo ya kipekee.

Siku chache zilizopita, Butita alikuwa ametumia akaunti zake za mitandao ya kijamii kutangaza habari za kusisimua kuhusu safari yake ya Marekani.

"Ninaondoka kuelekea Marekani leo. Asante Mheshimiwa Rais William Samoei Ruto kwa kunichagua kuandamana nawe katika ziara ya Kiserikali ya Marekani iliyoandaliwa na Rais wa Marekani Mheshimiwa Rais Joe Biden. Ukweli kwamba mimi ni sehemu ya Wajumbe wa Mkuu wa Taifa ni ishara tosha na tuna furaha kuwa tasnia ya ubunifu ni sehemu ya mazungumzo tutakayokuwa nayo katika safari hii.O.G.W," aliandika Butita.

Katika siku yao ya kwanza nchini Marekani Butita pia alishiriki video yake akishuka kutoka kwenye msafara wao wa magari akinukuu,

"Twende kazi, Siku ya 1 Rais William Ruto Ziara ya Nchi la Marekani🇺🇸🇰🇪 Kijana wako katika Msafara wa Rais Marekani."

Mkuu wa Nchi anatarajiwa kukutana na viongozi na mastaa mbalimbali wakubwa wakati wa ziara yake nchini Marekani, na Butita atakuwa akiwakilisha Uchumi wa Ubunifu.

Rais Ruto pamoja na wajumbe wake walitembelea kampuni maarufu ya utayarishaji filamu, Tyler Perry Studios ambapo alipaswa kukutana na Tyler Perry.

Butita, rais na wajumbe wengine pia walikutana na mtangazaji maarufu wa TV na mfanyabiashara Steve Harvey.