Ajali ya nyota wa Nigeria Junior Pope ilivyoilazimu Nollywood kuzingatia usalama

Ili kuboresha mambo, imependekeza kwamba chombo cha kudhibiti usalama kinapaswa kuanzishwa.

Muhtasari

•Mtayarishaji wa filamu hiyo, Adanma Luke, alisema aliambiwa kulikuwa na jaketi la kuokoa maisha na Pope Junior alipewa lakini hakulipokea.

•Mwigizaji Chidi Dike anasema kifo cha Pope Junior kilikuwa "mwamko kwa wote".

JUNIOR POPE.
JUNIOR POPE.
Image: HISANI

Ripoti ya awali kutoka Ofisi ya Uchunguzi wa Usalama ya Nigeria iliyotolewa mwezi uliopita iligundua mapungufu mengi.

Abiria huyo, mmoja wa watu wanane walionusurika, alikuwa ameleta jaketi la kuokoa maisha mwenyewe.

Katika video ambayo sasa imefutwa kwenye Instagram iliyochapishwa mara baada ya tukio hilo, mtayarishaji wa filamu hiyo, Adanma Luke, alisema aliambiwa kulikuwa na jaketi la kuokoa maisha na Pope Junior alipewa lakini hakulipokea.

“Nimeumia sana. Nimekuwa wa baridi sana. Jambo hili lote bado ni kama ndoto kwangu. Natamani ningeamka kutoka kwenye ndoto hii,” alisema kwenye video hiyo.

Baadaye aliandika: “Moyo wangu umevunjika vipande vipande ninapoandika haya… najikuta nikiomba, tunawezaje kurudisha nyuma wakati?”

Ruth Kadiri, mwigizaji mkuu, mtayarishaji na mtunzi wa filamu ambaye alimfahamu vyema Pope Junior, anasema alikuwa mtu wa ''furaha sana".

"Kila mara alileta nguvu chanya ... na nadhani alipendwa sana na wote," aliiambia podikasti ya BBC What in the World kuhusu rafiki yake.

Aliendelea kusema kuwa matukio kama lile lililomuua Pope Junior ni ya kawaida sana huko Nollywood.

Kadiri anakumbuka tukio ambalo alikuwa karibu kuzama majini wakati wa kurekodi filamu na kumfanya afikirie juu ya hofu ambayo mwigizaji "lazima awe alihisi katika dakika za mwisho za maisha yake".

"Ilinibidi kurekodi bila kutumia jaketi za kujiokoa," anasema.

"Niliuliza timu ikiwa kila kitu kiko sawa na wakasema mtumbwi ulikuwa sawa. Kwa hivyo nilipanda mashua, wakaanza kupiga kasia, na mtumbwi ukaanguka tu mtoni."

Aliokolewa na mwenzake ambaye alimshika majini.

Nyota huyo ambaye ana wafuasi zaidi ya milioni sita wa Instagram, sasa anataka mabadiliko.

Hata hivyo, anasema anaelewa vishawishi kwa waigizaji wanaotaka kuendelea kufanya jambo ambalo huenda si salama.

"Sote tunafanya mambo ya ajabu kwa ajili ya kupenda kazi hii. Tunafanya mambo ambayo kwa kawaida hatungefanya.

“Unapokua, unajifunza kuweka mahitaji yako kwanza. Sio kwa sababu haupendi kazi hii bali ikiwa kitu kitakwenda vibaya, ndio mwisho wake.

Kadiri anasema kuwa usalama ni suala la sekta nzima lakini wakati uzalishaji mkubwa, unaofadhiliwa vizuri unaweza kuchukua hatua, shughuli nyingi ndogo haziwezi kumudu gharama za ziada.

Ili kuboresha mambo, anapendekeza kwamba chombo cha kudhibiti usalama kinapaswa kuanzishwa ambacho kinaweza kuwa na watu kwenye maeneo ya kurekodi filamu.

Mwigizaji Chidi Dike anasema kifo cha Pope Junior kilikuwa "mwamko kwa wote".

Anakubali kwamba "usalama haujachukuliwa kwa uzito sana", lakini anabainisha kuwa kumekuwa na uboreshaji fulani.

Amegundua kuwa waongozaji na watayarishaji sasa wanajaribu kuhakikisha kuwa upigaji picha haupiti usiku sana, jambo ambalo hapo awali lilikuwa na maana ya safari za usiku.

“Kila kitu ni hatari... kuendesha gari kwa kasi sana. Kuna wakati mmoja nilichelewa kurudi nyumbani na nusura nipate ajali,” aliiambia BBC.

"Lakini ni bora sasa."

Ni urithi usiotarajiwa kwa mwigizaji anayeendelea na orodha kubwa ya filamu, lakini video ya mwisho ya Pope Junior inaweza kugeuza Nollywood kuwa mahali salama pa kufanya kazi.