Diana Marua alivyolazimika kuwa mama kwa dada zake akiwa mdogo baada ya wazazi kutengana

Wazazi wa Diana walitengana alipokuwa na umri wa miaka sita huku dadake mdogo akiwa na miezi sita.

Muhtasari

•Diana alizungumza kuhusu jinsi ilivyokuwa ngumu kwao wakati wa kukua na changamoto nyingi alizokabiliana nazo shuleni.

•Diana alifichua kuwa hakupata fursa ya kujenga uhusiano mzuri na mama yake kwani alifariki mara tu baada ya yeye kumaliza sekondari.

Image: INSTAGRAM// DIANA MARUA

Mke wa mwimbaji Kelvin Bahati, Diana Marua amefunguka kuhusu athari mbaya ambayo kutengana kwa wazazi wake kulikuwa nayo kwa yeye na dada zake.

Wazazi wa Diana walitalikiana miaka mingi iliyopita alipokuwa na umri wa miaka sita hivi. Mwanavlogu huyo na dada zake wawili waliachwa chini ya uangalizi wa baba yao.

Katika taarifa yake Jumatatu jioni, alizungumza kuhusu jinsi ilivyokuwa ngumu kwao wakati wa kukua na changamoto nyingi alizokabiliana nazo shuleni.

"Baada ya Wazazi Wangu Kutalikiana 💔 Mama yangu alituacha chini ya uangalizi wa Baba yetu, nilipokuwa na umri wa miaka 6 hivi, dada yangu mdogo @mitch_ngoje alikuwa na umri wa miezi 5 hivi," Diana alisimulia.

Aliendelea, “Maisha yetu tulipokuwa tukikua yalikuwa mabaya. Nilikuwa mwanafunzi niliyefanya vibaya zaidi katika mkondo wangu, kwenda shule ilikuwa mateso, nilikuwa naadhibiwa kwa kutofanya vizuri, nakumbuka niliaibishwa shuleni, nilipelekwa darasa la 3 kutoka la 8 kufundishwa takwimu na wadogo zangu, niligeuzwa kuwa kicheko, ambapo nyumbani, nilikuwa Mama kwa dada zangu, nilikuwa mpishi na yaya kwa wakati mmoja.”

Mama huyo wa watoto watatu aliendelea kufunguka kuhusu kukumbana na vipigo vingi nyumbani hadi kufikia hatua ya kutaka kutoroka. Hata hivyo, hangeweza kutoroka kwani aliwajali dada zake wadogo.

Alifichua kuwa hakupata fursa ya kujenga uhusiano mzuri na mama yake kwani alifariki mara tu baada ya yeye kumaliza elimu yake ya sekondari.

“Hatukuwa na uhusiano na Mama yetu na muda mfupi tu baada ya kumaliza shule ya upili, nilijua tungelipiza miaka iliyopotea, na kisha yeye akaaga dunia mwaka mmoja baadaye, nilimuuliza Mungu… KWA NINI SASA????  Ninapofikiria siku hizi, ninakumbuka maumivu na huzuni. Nisingependa mateso haya kwa mtoto yeyote anayekua," alisema.

Mwanavlogu huyo wa YouTube alimalizia kwa kutoa shukrani zake kwa Mungu kwa kumfuta machozi na kumpa familia ambayo anailea katika mazingira bora.

"Mungu asante kwa kunifundisha jinsi ya kuwapenda watoto wangu bila masharti. Jinsi ya kuwapa umakini na upendo ambao sikuwahi kupata. Uponye moyo wangu, nisaidie kusamehe na kuachilia 🙏🏼,” alisema.