Stevo Simple Boy amwagiza Kiengei kuomba msamaha, atishia kuhamasisha Wakenya kugoma

"Akikosa kuomba msamaha, nitaambia Wakenya wenzangu tugome, haki itendeke," Stevo alisema.

Muhtasari

• Stevo ambaye jina lake halisi ni Stephen Otieno Adera alimshtumu kasisi huyo kwa kumdhalilisha yeye na talanta yake.

•Stevo aliendelea kuwasihi Wakenya wenzake kumsaidia kudai haki kwani alihisi kukerwa na matamshi ya askofu Kiengei.

Stevo Simple Boy na Bishop Ben
Image: HISANI

Msanii mashuhuri kutoka Kibera Stevo Simple Boy ametaka mchungaji wa kanisa la JCM Benson Gathungu almaarufu Muthee Kiengei aombe msamaha.

Akizungumza na mwandishi wa habari za mitandaoni, Stevo ambaye jina lake halisi ni Stephen Otieno Adera alimshtumu kasisi huyo kwa kumdhalilisha yeye na talanta yake.

Mwimbaji huyo alilalamika kuwa badala ya mchungaji huyo kujikita katika kueneza neno la Mungu, alikuwa akiingilia maisha yake.

“Kwanza mchungaji Kiengei alisema mimi sina talent, nabweka kama mbwa, na naimba kama mbuzi. Sasa mimi nataka niambie Kiengei, badala afanye kazi ya Mungu, anakuja kuingilia maisha ya Stevo Simple Boy. Hiyo haifai, na yeye sio Mungu mwenye ameniumba,” Stevo alisema.

Stevo aliendelea zaidi kutoa makataa ya saa 24 ya kuomba msamaha kwa pasta huyo ambaye pia ni mtangazaji wa redio na msanii wa vichekesho vya Kikuyu.

“Nimempatia muda wa saa 24 akuje aombe msamaha pale Kibera, na asipoomba msamaha, basi Wakenya na wafuasi wangu tutagoma. Tutagoma tuandamane mpaka kanisa lake. Awache kunichezea. Hiyo ni kama amenidharau,” alisema.

Msanii huyo mcheshi aliendelea kuwasihi Wakenya wenzake kumsaidia kudai haki kwani alihisi kukerwa na matamshi ya askofu Kiengei.

"Akikosa kuomba msamaha, nitaambia Wakenya wenzangu tugome, haki itendeke," alisema.

Haya yanajiri takriban wiki moja baada ya Askofu Kiengei wa kanisa la JCM kukabiliwa na ukosaoaji mkubwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu maoni aliyotoa kuhusu Stevo Simple Boy na aliyekuwa mpenzi wake, muundaji wa maudhui Purity Vishenwa almaarufu Pritty Vishy.

Mchekeshaji huyo alilazimika kuomba msamaha baada ya Pritty Vishy kumtaka afanye hivyo akieleza kuwa maneno mabaya aliyotoa kumhusu yalimwathiri.

Jumanne wiki jana, mchungaji Kiengei alizamia kwenye mitandao yake ya kijamii na kuandika ombi la msamaha kwa mpenzi huyo wa zamani wa Stevo Simple Boy na kukiri kuwa alikosea kwa kauli alizotoa dhidi yake.

Kiengei alikiri kwamba alitaja jina la Pritty Vishy kwa njia isiyo sahihi na kwamba alivuka mipaka kwa kauli mbaya alizotoa.

“Prity Vishy, ​​samahani sana na nachukua muda huu kukuomba radhi sana kwa kutaja jina lako kwenye kipindi nilichopitia na kukutaja kimakosa, Pata nafasi moyoni mwako kunisamehe kwa kukuhutubia kwa njia isiyo sahihi, njia mbaya,” Kiengei alisema kupitia Facebook.

Mtumbuizaji huyo ambaye pia ni askofu katika kanisa moja maarufu jijini Nairobi aliahidi kutorudia kosa lilelile na akaendelea kumwalika Vishy kwenye kanisa lake.

"Hii haitatokea siku katika zijazo, naichukulia kama kosa langu, Pole dada yangu na karibu sana JCM CHURCH, KANISA LA WATU WOTE," alisema.