Jukumu kubwa ambalo mchekeshaji YY ameachwa nalo baada ya kumzika nyanyake

Nyanya ya mchekeshaji YY Comedian hatimaye alizikwa siku ya Ijumaa, Septemba 27.

Muhtasari

•YY alionyesha picha na video za tukio hilo lililojaa hisia na alionekana kuvunjika moyo kumuaga nyanya yake.

•"Kama mjukuu mkubwa, nina jukumu la kuweka urithi wa nyanya wa kuwaweka binamu pamoja," alisema.

Image: HISANI

Mama Zilpa Akech Ogola, nyanya ya mchekeshaji mashuhuri Oliver Otieno almaarufu YY Comedian hatimaye alizikwa siku ya Ijumaa, Septemba 27.

Marehemu Mama Zilpa alizikwa nyumbani kwake katika kijiji cha Kosele, kaunti ya Homa Bay katika hafla ya maziko iliyohudhuriwa na wanafamilia na watu wengine wa karibu.

YY alionyesha picha na video za tukio hilo lililojaa hisia kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii na alionekana kuvunjika moyo kumuaga nyanya yake.

“Mungu kuna mengi sana ya kikombe hiki. Niko tayari kwa lolote lile,”  YY alisema chini ya video iliyomuonyesha akiwafariji binamu zake.

Katika chapisho jingine, msanii huyo alionekana akiwa amekaa pamoja na wajukuu wengine wa marehemu na katika sehemu yamaelezo, akaahidi kuhakikisha umoja wa familia unaendelea.

"Kama mjukuu mkubwa, nina jukumu la kuweka urithi wa nyanya wa kuwaweka binamu pamoja," alisema.

Mchekeshaji huyo wa zamani wa Churchill Show alitangaza kifo cha nyanya yake katika chapisho la hisia mnamo Septemba 18.

Katika taarifa yake kwenye Instagram, aliomboleza marehemu na kukiri jukumu kubwa alilokuwa amecheza katika maisha yake.

“Nyanya yangu amepumzika. Pumzika vizuri Dani (Mama Zilpa Ogola). Umepigana vita chungu sana,” YY alisema katika tangazo lake wiki jana.

Aliongeza, “Asante kwa ushawishi wako katika elimu yangu. Dani atazikwa tarehe 27 Septemba 2024 katika kijiji cha Kosele. Nind Gi kwa Min Dolly."