
SOSHOLAITI Vera Sidika ametoa wito kwa mahoteli na migahawa kuwajali wateja wao haswa wanawake ambao wana umbile kubwa.
Kupitia kurasa zake kwenye Facebook na Instagram, Sidika
alieleza mafadhaiko na mateso ambayo watu wenye viuno vipana kama yeye hupitia
katika sehemu nyingi za starehe na burudani.
Alitoa ombi la kipekee kwa niaba ya wengine waliobarikiwa na
mwili kama yeye akitaka wamiliki wa mahoteli, migahawa na sehemu zingine za
starehe kutenga viti mahususi kwa ajili ya kukidhi mahitaji na starehe zao.
Mama huyo wa watoto wawili alijitokeza kama mwanaharakati wa
kutetea haki za watu wenye viuno vipana, akisema kwamba wengi wanateseka kwenye
sehemu za burudani na maadamu hawasemi, basi yeye atakuwa msemaji wao.
‘Mahangaiko ambayo
tunapitia huku nje sio mzaha. Jamani migahawa, tunahitaji viti vikubwa. Maisha ya
wasichana wanene yana umuhimu pia,” Sidika aliandika.
Ikiwa hilo halitoshi, aliambatanisha malalamiko yake na video
yake ya kuonyesha uhalisia jinsi yeye binafsi anateseka.
Sidika, ambaye katika video hiyo alionekana kwenye vazi la
rangi nyekundu aliingia katika mgahawa mmoja na kufanya majaribio ya kuketi
katika viti kadhaa lakini vyote vilionekana kumbana na kukera starehe yake.
Sidika si mwanamke mwenye umbile nene wa kwanza kulalamika
kuhusu wembamba wa viti vya sehemu za starehe kubana starehe zao.
Novemba 2024, mshawishi wa masuala ya usafiri kwa jina Jaelynn
Chaney alichukua kwenye TikTok kulalamikia mashirika ya ndege kuwatengea watu
wanene viti vyao spesheli.
'Hii haihusu kuwapa watu wanene zaidi - ni kuhusu kukidhi
mahitaji ya kimsingi.'
Influenza huyo wa usafiri wa ukubwa wa juu amehubiri kwa muda
mrefu kuhusu hitaji la viti vikubwa kwenye ndege, huku akidai kampuni kuu za
usafiri wa anga zinaendelea kupunguza viti na kusababisha msongamano wa abiria
zaidi.
Kwa mujibu wake, vipimo vya viti vya sasa mara nyingi
havifurahishi na wakati mwingine hata vinabagua abiria wakubwa, na kuwafanya
kuhisi kulazimishwa kununua viti vya ziada au kukabiliwa na usumbufu wakati wa
safari za ndege; suala hili mara nyingi huangaziwa na watetezi kwa kutumia
maneno "usawa wa mwili katika usafiri.".