
HARMONIZE amekiri kwamba aliumia sana kuona baadhi ya Kauli mitandaoni zikimtuhumu babake kwa uchawi baada ya yeye kuondoka katika lebo ya Diamond Platnumz, WCB.
Kulingana na Mwanzilishi huyo wa Konde Gang, babake ni mtu wa
dini sana na wala asingeweza kufikiria kuiendea WCB Wasafi kwa mganga ili
kuiponza baada ya mwanawe kuota mbawa.
Harmonize Alifichua kwamba mmoja kati ya watu ambao waliumia
sana alipoamua kuondoka kwa Diamond ni babake kwani muda wote alikuwa
anawachukulia kama ndugu.
“Katika vitu ambavyo
vilimuumiza sana babangu ni stori za mimi kuondoka WCB Wasafi. Mzee wangu
unajua kama nilivyosema ni mtu wa dini japo umri wake kidogo umesonga. Alikuwa anatuchukulia
mimi na Diamond kama watoto wake. Tulikuwa tuishi kama wasanii wa kufanya kazi
pamoja muda wote,” Harmonize alieleza.
Alisisitiza kwamba hata yeye mwenyewe asingekubali ushawishi
wowote wa kuiendea Wasafi kwa ushirikina, akitolea mfano wa jengo la msikiti
nyumbani kwao ambao aliupa jina la Diamond.
“Ni kama mimi
ninanavyoishi na Ibraah. Ndivyo ilivyokuwa kwa mimi na Diamond wakati huo. Kwa hiyo
kusema mzee wangu anaweza akawa anashiriki kwa namna yoyote kutengeneza
chochote kibaya kwa nia ya kuipoteza Wasafi sio kweli.”
“Mimi siamini hilo n
anaweza kupa tu mfano kidogo. Mliona Masjid, Msikiti ambao naujenga kule nyumbani
kwetu niliandika kwamba malipo ya kwanza ya kuanzisha ule msikiti alitoa
Diamond.”
“Sasa wewe unawezaje
kumfanyia uchawi mtu ambaye ametoa pesa yake ujenge msikiti kijijini kwako? Haileti
maana,” alisema.
Hata hivyo, alionekana kutowalaumu waliozalisha uvumi huo
akisema kwamba huenda ni kuchanganyikiwa kutokana na kutotarajia kwamba ukaribu
wake na Diamond ungefikia mwisho.
“Ni kama kule kutengana
kulikuwa kunamchanganya kila mtu kwamba inakuaje mbona hawa watu walikuwa
washikaji sana.”