Akothee azidiwa na hisia katika mazishi ya nyanyake , afichua kwa nini alikosa kuwatembelea muda mrefu

Alifunguka alivyoguswa sana na taarifa za kifo cha nyanyake, kiasi kwamba alishindwa kuzungumza juu yake.

Muhtasari

•Mama huyo wa watoto watano alichapisha picha zake kadhaa akiwa kwenye hafla ya mazishi, ambapo alionekana kuzidiwa na hisia.

•Akothee pia alichukua fursa hiyo kufichua jinsi kifo cha babu yake, takriban miaka saba iliyopita kilimuathiri.

Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Siku ya Alhamisi, Aprili 4, mwimbaji na mjasiriamali mashuhuri Esther Akoth almaarufu Akothee alihudhuria mazishi ya nyanyake wa kambo aliyeaga dunia hivi majuzi.

Mama huyo wa watoto watano alichapisha picha zake kadhaa akiwa kwenye hafla ya mazishi, ambapo alionekana kuzidiwa na hisia.

Alifunguka kuhusu uhusiano wake mzuri na marehemu, na jinsi alivyoonyesha upendo kwake alipokuwa hai.

“Bibi yangu wa kambo, mwanamke asiye na maneno mengi, alikuwepo kila mara nyumbani. Ingawa wakati fulani nilimkosa nyanya yangu wakati wa ziara zangu, nilijua mtu fulani angekuwepo kupokea vitu nilivyonunua kama angeenda kwenye hafla zake za SDA.

Ajuang, mwandani wake, alikua karibu naye baada ya kufariki kwa mumewe, James OGENDI Oyieko,” Akothee aliandika chini ya picha alizoshiriki kwenye Instagram.

Mwanamuziki huyo alifunguka jinsi alivyoguswa sana na taarifa za kifo cha nyanya yake, kiasi kwamba alishindwa kuzungumza juu yake.

“Kifo chake kilipofikishwa kwangu, nilijikuta nashindwa kuzungumza na mtu yeyote, hata mama yangu. Nilijitokeza tu kwenye mazishi, nikitoa heshima zangu,” alisema.

Aliongeza, “Kwa kweli, nilikuwa nimemwonyesha upendo wangu alipokuwa angali hai, nikimtolea maua yake. Anajua mapenzi yangu kwake. Upumzike kwa amani min oseyo.”

Akothee pia alichukua fursa hiyo kufichua jinsi kifo cha babu yake, takriban miaka saba iliyopita kilimuathiri.

Alizungumza jinsi ilivyomchukua takriban miaka mitatu kukubali hali hiyo, na jinsi alivyopata ugumu wa kuzuru nyumbani baada ya kifo.

“Kila nilipotembelea kaburi lake (babu yake) nilitokwa na machozi, kwani mawazo ya kutokuwepo kwake yalikuwa yakinilemea sana. Hakuwa babu tu; alikuwa rafiki yangu mkubwa, ndiye aliyenilea nilipokuwa nikikua, siku zote alikuwa na chai yake ya saa kumi na mbili asubuhi, isiyopingwa na nyingine yoyote. Ilinichukua miaka mitatu kukubaliana na kifo chake.

Hatimaye, nilijikusanya na kuanza kufanya safari za kuwatembelea nyanya zangu wawili. Ziara yangu ya hivi majuzi ilikuwa miezi miwili tu iliyopita, bila kujua kwamba habari nyingine ya huzuni iliningoja,” alisema.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani na Utawala wa Kitaifa, Raymond Omollo pia alikuwepo wakati wa mazishi ya Alhamisi ili kuomboleza na familia.